Naples, Italia
Mmiliki na mwenyekiti wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis amesema kwamba klabu yake haitosajili tena wachezaji wa kutoka Afrika hadi hapo wachezaji hao watakapokubali kutoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).
Beki Msenegali, Kalidou Koulibaly ambaye kwa sasa anaichezea Chelsea na kiungo Mcameroon, Andre Zambo walikosa mechi kadhaa za Napoli wakati wakiziwakilisha nchi zao kwenye fainali za Afcon ambazo zilifanyika kati ya Januari na Februari mwaka huu.
“Au vinginevyo wasaini kujitoa kushiriki katika Afcon,” alisema De Laurentiis kauli ambayo Koulibaly aliijibu akionyesha kusikitishwa na msimamo wa bosi wake wa zamani.
“Ni lazima uonyeshe heshima kwa timu ya Taifa kwa sababu huwezi kuzizungumzia timu za Taifa katika namna hii,” alisema Koulibaly.
“Nikiwa ndiye nahodha wa timu ya Senegal nafikiri hiyo si namna nzuri ya kuzizungumzia timu za soka za Afrika lakini namheshimu kama anafikiri timu inaweza kucheza bila ya wachezaji wa Afrika hiyo ni juu yake, si kila mtu ana mtazamo kama wake katika klabu,” aliongeza Kaulibaly.
De Laurentiis ambaye ni mtayarishaji filamu, pia aliipinga michuano iliyotaka kuanzishwa ya European Super League ambayo ilipingwa na wengi akiitaja kuwa ni michuano ya klabu zilizoonekana kuwa na hadhi fulani kwenye soka.
“Huwezi kuanzisha ligi ya super club kwa kuhusisha wanachama wa klabu zenye hadhi ambao wanawaalika wengine, unahitaji kuwa na demokrasia na kuweka milango wazi kwa kila mmoja,” alisema.
Kimataifa Bosi Napoli hataki wachezaji Waafrika
Bosi Napoli hataki wachezaji Waafrika
Read also