Na mwandishi wetu
Vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga wamefanikiwa kukata tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuitandika Tabora United mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam, Complex jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo Yanga inaungana na timu za Coastal Union na Ihefu FC ambazo pia zimejikatia tiketi ya nusu fainali ya michuano hiyo ambayo sasa inajulikana kwa jina la Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya benki ya CRDB kuwa mdhamini.
Katika mechi ya Yanga ambayo ilianza mapema Jumatano hii, vinara hao wa Ligi Kuu NBC waliandika bao la kwanza katika dakika ya 35 mfungaji akiwa ni Stephanie Aziz Ki.
Mabao mengine mawili ya Yanga yalifungwa na Kennedy Musonda dakika ya 66 na Joseph Guede dakika nane kabla ya kutimia dakika tisini za mchezo.
Kwa upande wa timu nyingine, Coastal imefuzu nusu fainali baada ya kuilaza bao 1-0 Geita Gold FC wakati Ihefu FC imefuzu kwa ushindi wa penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0 na Mashujaa FC.
Katika mechi za nusu fainali Yanga inatarajia kuumana na Ihefu wakati Coastal wao wataoneshana ubabe na mshindi wa mechi kati ya Namungo FC dhidi ya Azam.
Soka Yanga, Coastal zatua nusu fainali FA
Yanga, Coastal zatua nusu fainali FA
Read also