Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo, George Mpole amesema kwa sasa anajifua vilivyo akifanya mazoezi mara mbili kwa siku kwa ajili ya kuwa sawa kuelekea msimu ujao.
Mpole (pichani) ambaye hivi karibuni alisema anafikiria kutafuta timu mpya baada ya hali ya kufutwa kwa Ligi Kuu ya DR Congo msimu huu kutomridhisha, anajiweka sawa pia hata kama ikitokea amehamia timu mpya aendane na kasi ya kikosi kipya.
“Kipindi hiki cha mapumziko, ligi zinaenda mwishoni nimekuwa najipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao maana si mbali, kwa sasa nimekuwa nikifanya mazoezi mara mbili kwa siku, mfano asubuhi naenda ‘gym’ na jioni nafanya mazoezi mengine ya mpira, lengo ni kujiweka sawa zaidi,” alisema Mpole.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Geita Gold alisema hiyo ni program ambayo alipewa kutoka Lupopo, hivyo amekuwa akiitumia na inamuweka vizuri zaidi kwa ajili ya kuhakikisha msimu ujao anaendelea pale alipoishia.
Mpole amewahi kukipiga Real Nakonde ya Zambia, Mbeya City, Polisi Tanzania kabla ya kung’ara msimu uliopita akiwa na Geita akiibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 17 akimbwaga Fiston Mayele aliyeshika nafasi ya pili kabla ya msimu huu kutimkia Lupopo.