Munich, Ujerumani
Ujerumani, wenyeji wa fainali za Kombe la Ulaya 2024 ‘Euro 2024’ wamezianza fainali hizo kwa kishindo kwa kuinyuka Scotland mabao 5-1 au mkono katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa Ijumaa hii mjini Munich.
Ushindi wa Ujerumani bila shaka unaibua mtazamo mpya kwa timu hiyo inayonolewa na Julian Nagelsmann ambayo kabla ya kuanza fainali hizo ilionekana kudharauliwa na sasa huenda ikaingia katika timu zinazoweza kubeba taji.
Ujerumani ambao ni mabingwa mara tatu wa taji hilo walianza kuzitikisa nyavu za Scotland mapema kipindi cha kwanza kwa mabao ya Florian Wirtz, Jamal Musiala na Kai Havertz kwa penalti na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa 3-0.
Scotland ambayo ilibaki na wachezaji 10 uwanjani baada ya Ryan Porteous kupewa kadi nyekundu, ilipata bao la kujifariji baada ya Antonio Rudiger kujifunga wakati mabao mengine ya washindi yalifungwa na Niclas Fullkrug na Emre Can.
Akizungumzia ushindi huo Nagelsmann alisema kwamba ana furaha kwa sababu si rahisi kupata ushindi katika mechi ya kwanza ukiwa kwenye nchi yako.
Scotland, timu inayonolewa na kocha Steve Clarke inaweza kuonekana imejiweka pagumu na kupoteza matumaini baada ya matokeo hayo lakini bado ina mechi mbili za kufufua matumaini.
Ina mechi dhidi ya Switzerland itakayopigwa Jumatano na kufuatiwa na mechi nyingine dhidi ya Hungary ambayo itapigwa Jumapili, ni mechi ambazo inaweza kuzitumia vizuri na kuhakikisha haiziagi mapema fainali za Euro 2024.
Kimataifa Ujerumani yaipiga mkono Scotland
Ujerumani yaipiga mkono Scotland
Read also
