Na mwandishi wetu
Wakati Azam FC ikitua leo jijini Ndola, Zambia, timu ya Simba SC kesho inatarajiwa kutua Zanzibar ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi yao ya mechi za michuano ya Afrika zinazowakabili.
Azam imetimkia Zambia kwa ajili ya mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo huku kocha wa timu hiyo, Denis Lavagne akiamini hicho ni kipimo sahihi kwao kuelekea kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo yenye maskani yake Chamazi, Dar es Salaam itaumana na Al Akhdar ya Libya kwenye hatua ya pili ya awali ya michuano hiyo mnamo Oktoba 7 kabla ya kurudiana Oktoba 14, mwaka huu.
Kocha wa Azam, Denis Lavagne amesema: “Kwenye hii mechi jambo la kwanza muhimu ni mimi kuwajua zaidi wachezaji wangu, mazoezi ni mazuri lakini mechi ni kitu cha tofauti kabisa, kwa hiyo ni muhimu kwangu kuwajua na wachezaji ambao hawakucheza mechi ya Mbeya niwaone vizuri.
“Lakini pia kuimarisha uchezaji wa timu, nadhani Mazembe ni timu nzuri kujiandaa na Shirikisho, ni muhimu kucheza na timu nzuri ili kuwa na utimamu unaofanana na Kombe la Shirikisho ili kujiweka sawa kimashindano kwa sababu tunakaa siku 17 bila kucheza kwa hiyo ni muhimu kuwatafutia mechi wachezaji ili wawe na utimamu wa kimashindano.”
Upande wa Simba ambayo itaumana na Primeiro de Agosto ya Angola kwenye hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanaelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiweka fiti kwa kucheza mechi mbili za kirafiki.
Wekundu hao wakiwa huko watacheza mechi dhidi ya Kipanga, Septemba 25 kabla ya kucheza mchezo wake wa pili Septemba 27 na timu itakayowekwa wazi hapo baadaye na kisha kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam Septemba 28, mwaka huu.
Wakati timu hizo mbili maarufu za Dar es Salaam zikijichimbia maeneo hayo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wenyewe wataendelea kusalia Avic Town, Kigamboni jijini Dar esn Salaam kujiweka sawa kuwavaa Al Hilal ya Sudan kwenye hatua ya pili ya awali ya Klabu Bingwa Afrika.
Mwisho.
