Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema michuano ya Ngao ya Jamii imekuwa kipimo kizuri cha kujua timu yake ikoje kuelekea Ligi Kuu ya Wanawake inayotarajiwa kuanza Desemba 20, mwaka huu.
Simba Queens imefanikiwa kuwa mabingwa wa kihistoria baada ya kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga JKT Queens kwa penalti 5-4 baada ya kumaliza dakika 90 kwa suluhu katika fainali iliyochezwa Uwanja Azam Complex, Dar es Salaam jana jioni.
Mgunda amelipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuandaa mashindano hayo kwani yamempa kipimo kizuri kwa timu yake.
“Nashukuru kwa kuwa bingwa kwani mashindano yalikuwa magumu na yametufanya tujue tunajiandaaje maana JKT Queens ndio washindani wetu kwenye ligi hivyo nao wamejua wajiandae vipi kwa ajili ya ligi,” alisema.
Kocha wa JKT, Ester Chabruma alisema baada ya matokeo hayo, sasa wanaenda kujiandaa na ligi ili watetee taji lao kwa kufanya marekebisho kwenye makosa yaliyowagharimu.
“Mchezo ulikuwa mgumu na matokeo ndio hayo, sasa hivi tunaangalia mbele kwenye ligi tukianza kufanyia maboresho makosa yaliyotufanya tukose ubingwa wa Ngao ya Jamii,” alisema Chabruma.
Katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu nne, wachezaji wa Simba, kiungo Vivian Corazone alichaguliwa mchezaji bora wa michuano na kipa Carolyene Rufa akiibuka golikipa bora wa michuano hiyo huku Stumai Abdallah wa JKT akitajwa kuwa mchezaji bora wa mchezo wa fainali.
Soka Mgunda asifu Ngao ya Jamii
Mgunda asifu Ngao ya Jamii
Read also