Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya soka la ufukweni imeshika nafasi ya tatu katika michezo ya pili ya ufukweni iliyofanyika Hammamet nchini Tunisia kuanzia Juni 24 na kumalizika jana Ijumaa.
Mabingwa katika mashindano hayo ni Morocco walioifunga Senegal kwa penalti 4-3 baada ya kumaliza mchezo kwa sare ya 3-3 na kuwafanya Senegal kuwa wa pili, Kenya ikishika nafasi ya nne na Libya wa tano.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tunisia, timu ya Tanzania inayonolewa na beki na nahodha wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawassa, katika mchezo wake wa mwisho uliochezwa juzi iliifunga Libya mabao 9-3.
“Tunashukuru Mungu tumemaliza mashindano yalikuwa mazuri na yametufundisha, vijana wamezidi kuimarika na wamepambana kuhakikisha wanapeperusha bendera ya taifa vizuri na leo tumeanza safari kurejea nyumbani na tunatarajia kufika huko saa 5:00 usiku,” alisema Pawassa.
Wakati timu ya soka ikirudi na medali za shaba, wanariadha wa Tanzania hawakurudi na medali yoyote kwani mwanariadha, Joseph Panga alimaliza wa nne katika mbio za kilometa 10 kwa kutumia dakika 29:33 na Asha Salum akaambulia nafasi ya saba akitumia dakika 37:17.
