Na mwandishi wetu
Kuelekea mchezo wa Watani wa Jadi, Simba na Yanga Jumamosi hii, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeeleza kuwa ulinzi madhubuti umeanza kuimarishwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam utakapopigwa mchezo huo.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi jijini Dar na Ofisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda akifafanua kuwa tayari wamezungumza na watu wa ulinzi na usalama ili kuweka usalama kwenye mchezo huo ambao huhudhuriwa na mashabiki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Niseme tu kwamba hadi sasa tumezungumza na watu wa ulinzi juu ya kudhibiti matukio mbalimbali kwenye mchezo huo mkubwa Afrika Mashariki na Kati na mambo hayo yanakwenda vizuri kuhakikisha ulinzi madhubuti wa hadhi ya mchezo huo unakuwepo,” alisema Boimanda.
Pia, Boimanda alifafanua kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani, mbali na wanaokata tiketi kawaida ambapo alisema: “Kutakuwa na mialiko ya watu maalumu ambao watapewa kadi kwa mtu husika na watoto nao wataingia kwa kutumia kadi vilevile.
Boimanda hata hivyo alisema kwamba kadi hizo zitatumika kwa walengwa tu na kama mlengwa atashindwa kuhudhuria basi atoe taarifa ili utaratibu mwingine uendelee lakini kadi yake haitatumika na mtu mwingine yoyote.”
Katika mchezo huo wa 112 wa ligi kuu baina ya timu hizo, Yanga itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkapa unaoingiza mashabiki 60,000 na kutokana na wingi wa mashabiki, ulinzi huimarishwa ili kuepuka vurugu na kuweka sawa mambo mengine ya kiusalama.
Soka TPLB waimarisha ulinzi Kwa Mkapa
TPLB waimarisha ulinzi Kwa Mkapa
Read also