Na mwandishi wetu
Imewekwa wazi kuwa mwamuzi Alhadi Mahamat (pichani) ndiye atakayeamua mechi ya mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Al Ahly ya Misri na Simba SC ya Tanzania.
Mahamat, 37 raia wa Chad ndiye aliyewahi kuichezesha Yanga pia ilipopoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouzdad katika mchezo wa hatua ya makundi uliopigwa nchini Algeria.
Mwamuzi huyo sasa ndiye atakayewaamua Simba katika mchezo wao huo utakaounguruma kesho Ijumaa mjini Cairo, Misri kuanzia saa 5 usiku.
Kwa mchanganuo Simba inapaswa kuwa waangalifu kinidhamu kwani mwamuzi huyo katika mechi zake nane zilizopita ametoa kadi za njano 28 ikiwa ni wastani wa kadi tatu kila mchezo huku akitoa kadi nyekundu moja.
Mahamat alitoa kadi nyekundu katika mchezo wa michuano ya African Football League (AFL) baina ya Enyimba na Wydad AC ambao Enyimba ilichapwa bao 1-0, Oktoba 22, mwaka jana.
Katika mchezo huo, Simba inahitaji ushindi ili kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kwenye mchezo wa awali uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Kimataifa Mahamat ndiye mwamuzi Simba, Ahly
Mahamat ndiye mwamuzi Simba, Ahly
Read also