Na mwandishi wetu
Baada ya kipa wa Simba, Aishi Manula kukosa tuzo ya msimu uliopita wa 2021/22, amefunguka kuwa hayo yametokana na kutofanya vizuri kwa timu yake ya Simba.
Kwenye tuzo hizo, Manula alikuwa akiwania kipengele cha Kipa Bora wa Ligi Kuu ambayo ilikwenda kwa Djigui Diarra wa Yanga lakini pia akakosekana kwenye kikosi bora cha msimu ambacho amekuwa akiwemo kwa misimu mfululizo iliyopita.
Akilizungumzia hilo, Manula alisema kwa ujumla Simba ilishindwa kutimiza ambayo walijiwekea ndiyo maana kumekuwa na matokeo ya tofauti msimu huo na kukiri kuwa msimu haukuwa mzuri kwao hata kidogo.
“Niseme msimu ulikuwa mzuri, ulikuwa wa ushindani kwa bahati mbaya kama klabu hatukuweza kupata tulichostahili au malengo tuliyojiwekea. Kiujumla kama klabu ilikuwa na msimu mbaya ndiyo maana kumekuwa na matokeo kama haya.
“Japo msimu ulikuwa wa ushindani lakini kwetu ulikuwa msimu mbaya kwa sababu sio vile tulivyozoea. Kama klabu na wachezaji tuliweka nguvu kubwa kwenye mashindano ya kimataifa, tuliona kwamba tunapiga hatua zaidi ukitofautisha na misimu uliyopita lakini hatukuweza kufanikiwa,” alisema Manula.
Licha ya kukosekana kwa Manula lakini ni wachezaji watatu pekee walioingia kwenye kikosi bora cha ligi msimu huu ikiwa ni tofauti na msimu uliopita, wachezaji saba wa Simba waliingia kwenye kikosi hicho.
Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mchezo wameingiza wachezaji sita kwenye kikosi hicho, Djigui Diarra, Djuma Shabani, Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala, Feisal Salum na Fiston Mayele. Wengine Mohamed Hussein, Henock Inonga, Pape Sakho (Simba), Abdul Selemani (Coastal Union) na George Mpole wa Geita Gold.
