Na Hassan Kingu
Stephane Aziz Ki amefunga bao ambalo limemheshimisha, limeiheshimisha Yanga na mashabiki wake, limedhihirisha thamani yake na kwa nini mabosi Yanga walipambana na kuwa tayari kutoa mamilioni ili tu kumsajili mchezaji huyo.
Bao alilofunga si tu ni aina ya bao ambalo mashabiki wanaliita kuwa ni ‘bao tamu’, bali amefunga bao la hadhi ya juu, kwenye mechi muhimu yenye hadhi ya bao hilo, ni mechi muhimu, kubwa inayoteka hisia za mashabiki ndani na nje ya nchi, ni Dar Derby au Kariakoo Derby. Ni aina ya vitu ambavyo mchezaji kutoka nje ya nchi anatakiwa aifanyie klabu ili kulinda heshima yake.
Kuna mashabiki wengi ambao kama si bao la Aziz Ki pengine leo Jumatatu ingekuwa siku ngumu mno kwao, kama baada ya dakika 90 ubao ungesomeka Yanga 0- 1 Simba, kuna ambao wangelazimika kuficha sura zao, wengine wangekuwa wanahesabu hasara ya matokeo mabaya kwenye michezo ya kubahatisha, wengine wangekuwa wakizifikiria na kujutia ahadi walizowekeana na watani wao.
Kwa bao la kusawazisha alilofunga, Aziz Ki na matokeo kusomeka Yanga 1-1 Simba ni kama kapambana na kuhakikisha anadhihirisha thamani yake ndani ya Yanga na kuifanya iendelee kuwa juu. Katika klabu ya Manchester United kuna beki wa bei mbaya, anaitwa Harry Maguire, huyu kwa sasa anahaha kuitafuta thamani yake katika klabu hiyo.
Mwaka 2017 alinunuliwa kwa kiasi kinachodaiwa kufikia Pauni 80 milioni kutoka Leicester City, ni usajili wa rekodi kwa beki, na kutokana na uwezo wake miezi sita baadaye akawa nahodha wa timu, lakini tangu msimu huu uanze mambo yake yamekuwa hovyo, ameshapoteza nafasi kikosi cha kwanza, hata alipopewa nafasi alijikuta akizomewa na mashabiki kwa kucheza chini ya kiwango.
Thamani ya Maguire inazidi kushuka katika klabu na hapo hapo gumzo kubwa likawa ufinyu wa nafasi yake kwenye kikosi cha England kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia lakini jambo la kufurahisha ni kwamba mchezaji mwenyewe hana amani, anahaha kuitafuta thamani yake katika klabu hiyo.
Hivi karibuni beki wa Simba, Joash Onyango alijikuta akisugulishwa benchi na kocha Maki Zoran, jambo hilo lilimtesa na kumkosesha raha kiasi cha kutishia kuondoka katika klabu hiyo, hivyo ndivyo mchezaji anavyotakiwa kuwa hasa yule wa kigeni, wakati wote lazima thamani yake ionekane au ijidhihirishe na mwenyewe apambane kuhakikisha hilo linatokea.
Usajili wa Onyango ni ishara ya umakini mwingine wa mabosi wa Simba katika kusajili mchezaji kutoka nje ya nchi, kauli mbaya dhidi ya Onyango zilizokuwa zikitolewa kwamba ni mzee au ameshajichokea hazikuwasumbua Simba, wakashikilia msimamo wao na sasa wanaiona thamani ya mchezaji huyo tena kwenye mechi muhimu za Derby na zile za kimataifa.
Si vibaya kwa baadhi ya klabu za Ligi Kuu NBC kujiuliza kuhusu thamani ya wachezaji walio kwenye vikosi vyao hasa wale wanaosajiliwa kutoka nje ya nchi tena kwa bei mbaya, je wana thamani hiyo? Au wanafanya juhudi zozote kudhihirisha thamani yao? Au ni wachezaji wa kula mishahara.
Kwa klabu zinazoendeshwa kwa michango ya wafadhili, udhamini na hata kutembea bakuli au ambazo uwezo wao kifedha kiujumla ni mdogo na wa kutilia shaka, ni aibu kuwa na mchezaji aliyesajiliwa kwa bei mbaya kutoka nje ya nchi, ambaye analipwa vizuri lakini hana thamani aliyosajiliwa au haonyeshi juhudi zozote za kuitafuta thamani hiyo. Huyo mchezaji ni wa kuachana naye, bora kubaki na wazawa.
Aziz Ki ametuonyesha hilo kwa kufunga bao ambalo pia linaweza kuwa sababu ya kuzitoa klabu katika kusajili wachezaji wa mchongo kutoka nje, mchezaji wa kutoka nje ya nchi lazima ajitofautishe na yule mzawa, awe mwenye kudhihirisha vitu vilivyoifanya klabu imfuate nje.
Lazima afanye vitu ambavyo vitawafanya mashabiki si tu waione thamani yake bali pia wamkubali kwa kukifurahia kile anachokifanya uwanjani, hata ikitokea akafanya vibaya basi mashabiki wanakuwa na kitu cha kukumbuka au kuwasahaulisha kosa la siku za nyuma.
Bao alilofunga Aziz Ki la mpira wa mbali au adhabu kwenye Derby, si kitu kipya katika soka nchini, aliwahi kufanya hivyo beki wa zamani wa Yanga, Ken Mkapa aliitungua Simba kwenye Derby kwa bao la mbali, ni hivyo hivyo kwa beki wa zamani wa Simba, Mavumbi Omar naye aliitungua Yanga katika namna hiyo hiyo kwenye Derby na wengineo.
Ni mabao ambayo yamepatikana kwenye mechi kubwa, yamewaheshimisha wachezaji na kuonyesha thamani yao kwenye klabu na ni mabao ambayo yanaendelea na bila shaka yataendelea kukumbukwa na hata kujadiliwa kutokana na umuhimu wa mechi na ubora wa mabao hayo.
Aziz Ki naye jana Jumapili kwenye Dar Derby kwa kutumia vyema guu lake la kushoto, alijiheshimisha na kudhihirisha thamani yake, amefunga bao ambalo tutaendelea kulijadili miaka kadhaa ijayo huku tukiwapongeza walioona umuhimu wa kumsajili.