Manchester, England
Kiungo wa Man Ciy, Kevin De Bruyne, 33, ametangaza kuwa ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu wa 2024-25 baada ya kumalizika kwa mkataba wake na klabu hiyo.
De Bruyne (pichani) amekuwa mchezaji muhimu wa Man City tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2015 akitokea Wolfsburg ya Ujerumani na hadi sasa amebeba mataji 16 likiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema De Bruyne ni kati ya viungo bora waliowahi kucheza soka England na haingekuwa rahisi kwake kumwambia kwamba hatoendelea kuichezea Man City.
De Bruyne ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya Ubelgiji ameifungia Man City mabao 106 katika mechi 413 ingawa msimu huu kidogo haukuwa mzuri kwake kwani ameanza kipindi cha kwanza mechi 19 tu.
“Iwe tunataka au hatutaki, huu ni wakati wa kusema kwaheri,” alisema De Brunye kupitia mitandao ya kijamii.
De Bruyne alisema soka limemfikisha kwa watu wa Manchester na jiji la Manchester na hakuwa na la kufanya zaidi ya kuifukuzia ndoto yake bila kufahamu kwamba kipindi chote hicho kilikuwa cha kubadili maisha yake.
“Hawa watu wamenipa kila kitu, nami sikuwa na la kufanya zaidi ya kujitoa kwa kila kitu, nini kilitokea…Tulishinda kila kitu,” alisema De Bruyne.
Alisema yeye na familia yake Man City kutaendelea kuwa nyumbani kwao na hawezi kutoa shukrani za kutosha kwa jiji, klabu na maofisa wa klabu, wachezaji wenzake, marafiki na familia kwa safari ya kipindi cha miaka 10.
