Na mwandishi wetu
Baada ya Simba jana kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Haras El Hodoud katika mechi yao ya kirafiki, kocha mkuu wa timu hiyo, Zoran Maki amefurahishwa na matokeo hayo ambayo alisema yamemuonyesha mapungufu ya kikosi chake.
Hadi sasa Simba imeshacheza michezo mitatu, ikishinda mmoja, sare moja kabla ya kupoteza jana wakati wakiendelea na kambi yao jijini Ismailia, Misri wakijiweka sawa kwa msimu ujao.
Baada ya mchezo huo, Maki alisema ulikuwa mchezo bora sana tofauti na michezo miwili iliyopita dhidi ya Ismailia na Abo Hamad ambapo wamewapa upinzani mkubwa na hiyo imetokana na ukubwa wa timu yenyewe na kuwapa kipimo halisi.
“Sababu iliyofanya tupoteze mchezo ni mapungufu katika eneo la kiungo lakini pia vijana wangu hawakutengeneza nafasi za kutosha za kufunga,” alieleza Maki na kuongeza: “Timu ilicheza taratibu sana tofauti na falsafa yangu ambayo nimekuwa nikisisitiza mpira wa kasi ambao walifanya vizuri kwenye michezo iliyopita lakini kwenye mchezo huu imekuwa tofauti kidogo, nimebakiza michezo miwili ya kiufundi kabla ya kutoa ripoti kuhusu kikosi,” alisema Maki.
Simba inatarajia kurejea nchini Agosti 5 mwaka huu kwa ajili ya tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8 na kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa Agosti 13, mwaka huu.
Soka Kipigo Simba champa somo kocha
Kipigo Simba champa somo kocha
Read also