London, England
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ataendelea kudhihirisha hisia na mihemko anayokuwa nayo kwenye mechi licha ya kuwa tayari amepewa adhabu ya kufungiwa mechi moja.
Arteta atakosekana katika mechi ya leo Jumamosi ya Ligi Kuu England (EPL) kati ya Arsenal na Aston Villa baada ya kupewa kadi ya njano kwa mara ya tatu katika mechi ya ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Luton, Jumanne iliyopita.
Mwamuzi wa mechi dhidi ya Luton, Samuel Barrott alimpa Arteta kadi kwa kile kilichoonekana kuwa kocha huyo alifurahia kwa namna iliyopitiliza Arsenal ilipopata bao la ushindi lililofungwa na Declan Rice.
“Sijui namna ya kuacha, ni tukio lililoteka hisia kwa kila mmoja, kubadili matokeo na kujiwa na hisia za furaha na kujisahau upo wapi na hata eneo unalotakiwa kuwa,” alisema Arteta.
“Ni kwa bahati mbaya sasa siwezi kuwa pembeni ya timu yangu uwanjani lakini ni uamuzi ambao wameuchukua kwa kuangalia kanuni moja kwa moja,” alisema Arteta.
Ushindi huo umeiwezesha Arsenal kuendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa ligi hiyo yenye jumla ya timu 20.
Arteta huenda akakutana na adhabu nyingine ya kufungiwa kwa kosa la kutoa kauli ambazo Chama cha Soka England kimesema hazifai alipokuwa akilalamikia bao pekee na la ushindi walilofunga Newcastle katika mechi yao na Arsenal.
Bao hilo ambalo lilitokana na maamuzi ya kupitiwa kwa VAR, Arteta alisema kwamba kukubalika kwake ni aibu na fedheha katika EPL.