Na mwandishi wetu
Mshambuliaj wa Simba, Saido Ntibazonkiza ameeleza furaha yake kuchaguliwa mchezaji bora wa Simba mwezi Januari huku akiwaahidi mashabiki wa timu hiyo kuwa ataendelea kuwapa furaha zaidi.
Saido amechaguliwa mchezaji bora wa Simba akiwazidi mabeki Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ alioingia nao fainali.
Akieleza furaha yake hiyo, Saido alifunguka kuwa licha ya kuwashukuru wachezaji wenzake kwa kushirikiana naye uwanjani mpaka kutunukiwa tuzo hiyo lakini anafurahi pia kuona Simba inazidi kufanya vizuri hata baada ya kutua kwa Wekundu hao hivi karibuni.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha mpaka sasa na kupata tuzo hii, niwashukuru viongozi pia wachezaji wenzangu ambao tumeshirikiana pamoja maana bila wao nisingeonekana bora kiasi hiki.
“Nashukuru pia kuona timu inaendelea kufanya vizuri maana ilikuwa sababu ya mimi kuchukuliwa kwenye timu kuongezea nguvu, naomba Mungu niendelee kufanya vizuri na mashabiki wazidi kutuunga mkono tupo kwa ajili yao na tutaendelea kuwapa furaha,” alisema Saido.
Mchezaji huyo raia wa Burundi aliyetua Simba hivi karibuni kwenye usajili wa dirisha dogo la Januari, katika mwezi huo amecheza mechi tatu, akifunga mabao mawili kutoa pasi ya bao moja.
