Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imetangaza kuachana na kocha wake Manqoba Mngqithi wakati huo huo kukiwa na habari kuwa kocha huyo anahitajika katika klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Taarifa ya klabu ya Yanga iliyopatikana Jumamosi Oktoba 24, 2026 ilithibitisha kocha huyo kuachwa pamoja na kocha wa viungo, Chyna Mokaia.
Uamuzi wa klabu hiyo kuachana na Manqoba umefikiwa baada ya wiki kadhaa za uvumi kuhusu kutimuliwa kwake baada ya kufungwa mabao 2-1 na mahasimu wao Simba kwenye Ligi Kuu NBC.
Manqoba alijiunga na Yanga Julai mwaka huu akipewa matumaini makubwa lakini mwenendo na matokeo yasiyo ya kuvutia vimeonekana kuwakera mashabiki na viongozi wa timu hiyo.
Kabla ya kufukuzwa Manqoba alikuwa akilalamikiwa kwa upangaji mbovu wa timu, soka lisilovutia ingawa ameifikisha Yanga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na kubeba Ngao ya Jamii.
Wakati huo huo chanzo kimoja cha habari Afrika Kusini kimedai kuwa Manqoba ambaye pia amewahi kuzinoa timu za Mamelodi Sundowns na Lamontville Golden Arrows anatakiwa na klabu ya Kaizer Chiefs.
Kaizer Chiefs inadaiwa kuanza kumjadili kocha huyo mara baada ya kutimuliwa Yanga ikiamini anaweza kusaidia kuweka mambo sawa baada ya kuanza vibaya msimu wa Ligi Kuu Afrika Kusini.
Hii si mara ya kwanza kwa Chiefs kuhusishwa na kocha huyo ambaye pia anatokea nchini Afrika Kusini ingawa wakati wote mipango huyo haikuweza kukamilika.
Kimataifa Manqoba aachwa Yanga, atajwa Kaizer Chiefs
Manqoba aachwa Yanga, atajwa Kaizer Chiefs
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
