London, England
Winga Gareth Bale amekamilisha kitu muhimu katika maisha yake ya soka, ameiwezesha Wales kufuzu fainali za Kombe la Dunia baada ya miaka 64 hapo hapo akiacha swali la klabu gani anajiunga nayo.
Mchezaji huyo mwenye misuli na mashuti yenye kuzaa mabao, hivi karibuni aliaga rasmi Real Madrid akijigamba kwamba anafarijika kutimiza ndoto yake kwa kuichezea timu hiyo, na hapana shaka anafurahi kwa kutimiza ndoto ya pili ambayo ni kuiwezesha Wales kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Akiwa ndiye nahodha wa timu ya Wales, Bale anashikilia rekodi ya kuifungia mabao mengi timu hiyo, mabao 38 katika mechi 103 alizoichezea timu hiyo hadi sasa idadi ambayo hapana shaka itaongezeka wakati huu timu hiyo ikijiandaa na fainali za Kombe la Dunia wakati wa fainali zenyewe.
Awali Bale alinukuliwa akisema kwamba angestaafu kama Wales isingefuzu fainali za Kombe la Dunia lakini sasa jambo hilo halipo baada ya Wales kufuzu na ni dhahiri kwamba hawezi kukaa hivi hivi hadi Novemba, atalazimika kuwa na timu ya kuichezea kuanzia sasa iwe kwa mkataba mrefu au mfupi.
Timu ambazo tayari zimeonyesha ni ya kumtaka mchezaji huyo ni Cardiff City ambayo naye anatajwa kuvutiwa nayo lakini wako ambao wanaamini kwamba klabu hiyo ni sahihi kwake kwa wakati huu akiwa tayari ana miaka 32 na tayari mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo ya awali.
Hapo hapo pia kuna ofa ya kwenda Marekani kucheza soka katika ligi ya huko na kurudi klabu yake ya zamani ya Tottenham, yote hayo yamekuwa yakizungumzwa kuhusu mchezaji huyo ambaye katika miaka yake tisa na Real Madrid ametwaa mataji matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika klabu ya Cardiff kuna suala zima la mshahara, huenda hilo linaweza kuwa mjadala mpana kwani akiwa Real Madrid, Bale alikuwa akilipwa Pauni 600,000 kwa wiki, malipo ambayo yanazidi malipo ya wiki ya kikosi cha kwanza cha timu ya Cardiff.
Kwa vyovyote vile kama anaamua kwenda timu hiyo jambo moja litakalotokea ni kupunguziwa mshahara wake kwa kiasi kikubwa, itakuwa vigumu kwa Cardiff kumlipa mshahara kama wa Real Madrid au hata unaokaribia kufanana na huo.
Hivi karibuni aliuzwa na waandishi wa habari kuhusu ofa zilizomkononi mwake ni za timu gani, jibu la Bale lilikuwa fupi tu, “nina ofa kibao.”
Kimataifa Bale anaenda wapi baada ya Madrid?
Bale anaenda wapi baada ya Madrid?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
