Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Yanga umeahidi kuwafuturisha mashabiki 60,000 watakaoingia Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mchezo huo umepangwa kuanza saa tatu usiku na kwa kuwa Waislamu wapo katika ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wazi kuwa mashabiki wataanza kuingia uwanjani kuanzia muda wa futari saa 12:30 na kuendelea.
Ikumbukwe wiki iliyopita uongozi wa timu hiyo ulitangaza kuwaingiza bure mashabiki 48,000 wa viti vya mzunguko kushuhudia mchezo huo kama mkakati wa uongozi wa timu hiyo kuwapa zawadi mashabiki wao kwenye mchezo huo muhimu.
Akizungumza na vyombo vya habari, meneja wa habari na mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe alisema hayo yote wanayafanya kwa lengo la kutaka mashabiki wao wajae kwa wingi Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya kuishangilia timu yao.
“Ni mchezo ambao tumedhamiria kupata ushindi na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuingia nusu fainali, hivyo tumeona tuwafuturishe mashabiki wetu ambao tunaamini mpaka muda wa kawaida wa kufuturu wanaweza kuwa uwanjani tayari kwa mchezo huu muhimu kwetu,” alisema Kamwe.
Alisema si mara ya kwanza wao kuandaa chakula kwa mashabiki wao, walishafanya hivyo mara kadhaa ikiwemo kuwapa supu, hivyo kutoa futari kutawarahisishia mashabiki wao kujaa kwa wingi uwanjani na kuishangilia timu yao.
Yanga inasaka ushindi wake wa kwanza mbele ya Mamelodi ya Afrika Kusini ambayo mara ya mwisho walikutana kwenye michuano hiyo mwaka 2001 na Yanga kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 3-2 na mchezo wa marudiano Uwanja wa Kirumba, Mwanza walitoka sare ya 3-3.
