Na mwandishi wetu
Kocha wa KMC, Thierry Hitimana ameibuka na kumueleza mshambuliaji wake, Matheo Anthony anayeongoza kwa mabao Ligi Kuu NBC kwa sasa kuwa hapaswi kuwaza washindani wake katika kinyang’anyiro hicho la sivyo atapoteza mwelekeo wake.
Hayo yamezungumzwa na kocha huyo baada ya Anthony kufunga mabao manne na kumfikia kinara Reliants Lusajo wa Namungo huku wakifuatiwa kwa karibu na washambuliaji Fiston Mayele wa Yanga na Moses Phiri wa Simba waliofunga mabao matatu kila mmoja.
Hitimana ameeleza kuwa mapema ameshakaa na Anthony na kumueleza nini cha kufanya, acheze vipi na awe na malengo gani kama kweli anataka kufikia ndoto zake za kufanya vizuri na kutwaa kiatu cha ufungaji bora mwisho wa msimu.
“Siwezi kuzungumzia sana kuhusu ushindani wao lakini kwa upande wangu nimezungumza na Anthony nimemwambia kwamba ushindani sio mwepesi na anahitaji kujiangalia yeye kwanza kabla ya kujipa presha ya majina ya anaoshindana nao.
“Nimemuelekeza kuwa asikiwaze hicho kiatu maana ataanza kujipa mitihani na mwisho atatoka kwenye mstari wake, cha msingi atulie na kuendelea na mazoezi ya kufanya vizuri na kuisaidia timu kila siku na mwisho ataendelea kuongezeka kiwango na uwezo, ndivyo ninavyoweza kusema kuhusu hilo,” alisema Hitimana.
Anthony alianza kufungua akaunti yake ya mabao kwenye mechi ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Polisi Tanzania na kisha kufunga mfululizo bao moja kwenye mechi mbili za mwisho na kuibua ushindani mpya kwenye kinyang’anyiro hicho.
Soka Hitimana amtaka Matheo asiwaze ufungaji bora
Hitimana amtaka Matheo asiwaze ufungaji bora
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
