Na mwandishi wetu
Ikicheza na wachezaji 10 uwanjani, Azam FC imeibuka kidedea kwa kuichapa Yanga mabao 3-2 na kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB.
Matokeo ya mechi hiyo ya nusu fainali iliyopigwa Jumapili Juni 20, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, yanaifanya Yanga kulitema rasmi taji la michuano hiyo walilolimiliki kwa misimu minne.
Ushindi wa Azam kwa Yanga ulipatikana baada ya timu hizo kutoana jasho kwa dakika 120 huku Azam ikipata pigo dakika ya 70 baada ya beki wake Yoro Diaby kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Kadi hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Diaby kumchezea rafu Prince Dube wa Yanga lakini licha ya upungufu huo, Azam walifanikiwa kumaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 kabla ya kutumia dakika nyingine 30 kupata bao la ushindi.
Azam walianza kuzitikisa nyavu za Yanga dakika ya 27 kwa bao la Himid Mao ambaye pia ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kupewa tuzo na kitita cha Sh milioni 1 na wadhamini wa michuano hiyo, Benki ya CRDB.
Mao akionesha kiwango cha juu kwenye mechi hiyo, alifunga bao hilo baada ya kuunganishiwa pasi na kiungo Jean Jacques Ngita.
Yanga walijibu mapigo kwa kusawazisha bao hilo kabla ya timu kwenda mapumziko mfungaji akiwa ni Dube baada ya kuunganishiwa pasi na Allan Okelo.

Azam walionesha umakini kwa kufunga bao la pili katika dakika ya 85 licha ya kuwa 10 uwanjani, bao lililofungwa na Elias Lawi aliyeutumia mpira wa kona uliopigwa na nyota wa zamani wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alifufua matumaini ya timu yake alipofunga bao la kusawazisha akiitumia pasi ya Okello na ndipo dakika 30 zilipoongezwa baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika matokeo yakiwa sare ya mabao 2-2.
Walikuwa ni Azam walioneemeka na dakika hizo kwa kufunga bao la tatu lililowekwa kimiani dakika ya 112 na Japhet Kitambala aliyeneemeka na makosa ya beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca.
Azam sasa inasubiri kucheza mechi ya fainali na Simba ambao katika mehi nyingine ya nusu fainali waliichapa Coastal Union ya Tanga mabao 4-0.
