Jonathan Haule
Simba imemtangaza Zoran Manojlovic kutoka Serbia kuwa kocha wao mkuu akichukua nafasi ya Pablo Franco ambaye ametimuliwa hivi karibuni. Tofauti na makocha wengi wapya wanaopokewa kwa mbwembwe, Zoran kwa bahati mbaya amejikuta akiwa mjadala kwenye mitandao.
Kibaya zaidi ni kwamba mijadala mingi kuhusu Zoran si yenye afya kwake, wengi wanaochangia mada katika makundi mbalimbali mitandaoni wameuanika wasifu wake na kumtaja kuwa ni kocha ambaye amekuwa akikaa na timu kwa muda mfupi na wengine kumuona kuwa ni mzee.
Na ingawa Pablo naye wasifu wake unaonyesha kuwa hakuwa kocha wa kukaa muda mrefu kwenye timu lakini yeye alipokewa kwa mbwembwe na baadhi ya vyombo vya habari vilimtaja kuwa ni kocha wa mataji lakini bahati mbaya Simba ilishuhudiwa ikipoteza mataji yeye akiwa kocha.
Wakati Pablo anakuja suala la kukaa kwenye timu muda mfupi halikuwa kubwa na wala halikusumbua sana watu lakini akapambwa na sifa kemkem ikiwamo kuwahi kuwa kocha Real Madrid hadi kuitwa kocha wa mataji na hapo ndipo unapoweza kujiuliza kwanini kwa Zoran sifa ya kutokaa na timu muda mrefu imekuwa nongwa.
Kati ya mijadala niliyoifuatilia kwa karibu sijaona zikichambuliwa kwa kina sababu hasa za kocha huyo kutodumu muda mrefu au kuachana na timu, haikuwa hivyo kwa Pablo na kwa Zoran si hivyo tofauti ni kwamba kwa Zoran kutodumu muda mrefu kwenye timu kumepewa tafsiri ya moja kwa moja ya sifa mbaya na kuonyesha kama vile amekuwa na matatizo.
Amekuwa kocha wa Al Hilal ya Sudan kuanzia Oktoba 2020 lakini Aprili 2021 akaibukia Belouizad ya Algeria lakini Septemba 2021 aliibukia Saudi Arabia akawa kocha wa klabu ya Al Tai ambako alitimuliwa baada ya miezi minne na sasa yuko Simba.
Ni kweli rekodi hiyo si nzuri lakini haitoshi kuwa tathmini ya moja kwa moja kwamba hafai, tafsiri nyingine inaweza kuwa ni kocha mzuri kwani hakai muda mrefu bila kazi. Ni namna tu utakavyofanya tathmini ya kina na kujiridhisha kama uwezo mdogo na hafai au ana sifa zinazombeba na ndio maana timu zinamkimbilia.
Kuna usemi uliozoeleka kwamba makocha huajiriwa ili wafukuzwe, lakini si kila kocha anayefukuzwa anakuwa na matatizo au kashindwa kazi kuna wanaofukuzwa kwa matatizo mengine ya tofauti zao na viongozi hasa kuwa na misimamo ambayo viongozi hawakubaliani nayo.
Kwa wanaokumbuka jinsi James Siang’a alivyoondoka Simba, sababu ilikuwa ni tofauti zake na viongozi si kweli kwamba alikuwa kocha asiyefaa au alishuka uwezo, je tumejiuliza kwa Zoran huko alikotoka sababu hasa ilikuwa nini? Je ni kote alifukuzwa au kuna alikoamua kuondoka mwenyewe?
Kocha Mzambia Patrick Phiri aliwahi kuondoka Simba katika namna ya ajabu ajabu baada ya muda mfupi lakini ni Phiri huyo huyo aliyekuwa na rekodi ya kipekee Simba ya kumaliza msimu bila kupoteza mechi, sasa tungemjadili kwa kukaa Simba muda mfupi kama Zoran tungemuona hafai lakini kumbe kulikuwa na matatizo ndani ya Simba ambayo alishindwa kuyavumilia akaamua kuondoka.
Gazeti moja lilifanya mahojiano naye na kumuuliza sababu hasa ya kuondoka Simba baada ya muda mfupi na jibu lake likawa rahisi kwamba Simba ya wakati huo haikuwa katika mazingira mazuri kwake hivyo akaamua bora ajiondokee.
Makocha wanaoamua kujiweka kando baada ya kuona mambo hayaendi wanavyotaka ni wengi, iliwahi kuwa hivyo kwa Kostadin Papic akiwa kocha Yanga kuna wakati aliwahi kujiweka kando siku chache kabla ya mechi dhidi ya Simba baada ya kuona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, kilichotokea Yanga ikapewa kipigo kikali na Simba.
Zoran ni kocha mzoefu katika soka la Afrika amewahi kufanya kazi nchini Angola, Morocco, Sudan na Algeria na amewahi kufikia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ambayo Simba wanaisaka kwa udi na uvumba, wakati uzoefu huo unadhaniwa kuwa na maana kwa Simba wapo watu mitandaoni wanaomuona kocha huyo kuwa ni mzee (miaka 59) na Simba ilitakiwa iwe na kocha kijana.
Yote kwa yote, hatuna sababu ya kuharakisha kumfanyia Zoran tathmini zisizo na uchambuzi wa kina badala yake tumpe muda, siku zote muda ni hakimu mzuri.
Soka Kocha mpya Simba azua mijadala
Kocha mpya Simba azua mijadala
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
