Rabat, Morocco
Mashabiki wa Simba wana kila sababu ya kuwa na furaha kama ilivyo kwa wale wa Senegal baada ya wachezaji wao Pape Ousmane Sakho na Sadio Mane kuibuka vinara kwenye tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zilizotolewa usiku wa kuamkia leo mjini Rabat, Morocco.
Sadio Mane mchezaji wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa anaichezea Bayern Munich ya Ujerumani ametwaa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika wakati Sakho, mchezaji wa Simba ametwaa tuzo ya bao bora, wachezaji hao wote ni raia wa Senegal.
Mane sasa anakuwa mchezaji wa pili wa timu ya Taifa ya Senegal au Simba wa Teranga kutwaa tuzo hiyo akiwa ametanguliwa na El Hadji Diouf ambaye kama ilivyo kwa Mane naye aliwahi kuichezea Liverpool baada ya kuiwakilisha Senegal kwenye fainali za Kombe la Dunia 2002 zilizofanyika Japan na Korea Kusini ambapo timu hiyo ilifikia hatua ya robo fainali.
Mane katika kinyang’anyiro hicho amembwaga nyota mwenzake wa zamani wa Liverpool, Mohamed Salah na nyota mwenzake wa timu ya Taifa ya Senegal, Edouard Mendy ambaye ni kipa wa Chelsea.
“Nimefurahi kwa kutwaa tuzo hii, kuna wachezaji wengi wenye sifa za kubeba tuzo hii lakini mimi ndiye niliyechaguliwa, nimepewa heshima na namshukuru kila mtu kwa hili, huu ni mwaka mzuri wa Senegal,” alisema Mane mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo ikiwa ni mara ya pili kuibeba baada ya mwaka 2019 katika sherehe zilizofanyika nchini Misri katika mji wa Hurghada.
Tuzo hizo kwa kiasi kikubwa zilitawaliwa na Senegal ambapo kocha wa timu hiyo, Aliou Cisse naye alishinda tuzo ya kocha bora wakati Sakho wa Simba yeye aliinasa tuzo ya bao bora na hivyo kuwapa furaha mashabiki wa Simba. Tuzo hiyo imetokana na bao lake tamu ambalo alilifunga kwa staili ya tiki taka katika mechi ya Simba na Asec ya Ivory Coast ya Kombe la Shirikisho.
Mbali na tuzo hizo tatu, Senegal pia wametwaa tuzo ya timu bora ya mwaka na ile ya mchezaji bora mwanaume kijana wa mwaka iliyokwenda kwa kiungo wa Tottenham Hotspur, Pape Matar Sarrna ambaye alianza kuichezea Senegal akiwa na miaka 18 na alikuwamo katika kikosi kilichobeba Afcon 2021 na hivyo kuifanya nchi hiyo itawale hafla ya tuzo hizo kwa kuondoka na jumla ya tuzo tano.
Kwa upande wa wanawake, Asisat Oshoala wa Nigeria alitwaa tuzo ya mwanasoka bora mwanamke ikiwa ni mara yake ya tano kufanya hivyo akimbwaga Mnigeria mwenzake Perpetua Nkwocha wakati tuzo ya kocha bora mwanamke imekwenda kwa Desiree Ellis wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini au Banyana Banyana.
Tuzo ya klabu bora imekwenda kwa klabu ya Wydad ya Morocco ambao ndio vinara wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/22 wakati kwa upande wa wanawake tuzo hiyo imekwenda kwa timu ya wanawake ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni vinara wa ligi ya wanawake nchini mwao na ndio vinara wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.
Mshindi wa tuzo ya timu bora ya Taifa ya wanawake atatajwa baada ya mechi ya fainali ya Afcon kwa wanawake itakayopigwa Jumamosi hii kati ya wenyeji Morocco dhidi ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Moulay Abdellah mjini Rabat.
Kimataifa Mane, Sakho wang’ara tuzo CAF
Mane, Sakho wang’ara tuzo CAF
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
