Manchester, England
Man United inashika nafasi ya 13 katika Ligi Kuu England, imepoteza mechi tatu za awali za ligi hiyo, imechapwa mabao 4-3 na Bayern Munich katika Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag anasema wako pamoja licha ya kuuanza msimu vibaya.
“Najua si kila wakati utakuwa juu, kuna wakati mapengo yatajitokeza na hayo yanaweza kusaidia kukufanya uwe imara pale tu mtakapoendelea kuwa wamoja,” alisema kocha huyo Mholanzi.
“Hicho ndicho tunachokifanya kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, kwa maofisa wote na makocha, kila mmoja yuko pamoja na wenzake na tukiwa wamoja hapa United tunapambana pamoja,” alisema.
Msimu uliopita wa 2022/23 ulikuwa wa kwanza kwa Ten Hag katika kikosi cha Man United, alimaliza msimu huo timu yake ikiwa nafasi ya tatu kutoka ya sita waliyoishika msimu mmoja kabla.
Man United chini ya Ten Hag pia ilifanikiwa kubeba taji la Carabao pamoja na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo tayari wameinza kwa kupokea kichapo.
Katika msimu huu ambao ni wa pili kwa Ten Hag na Man United, kocha huyo amekiimarisha kikosi chake kwa kuwasajili mshambuliaji, Rasmus Hojlund, kiungo Mason Mount na kipa Andre Onana lakini hawajaweza kuuanza vizuri msimu huu.
Katika Ligi Kuu England Man United imepoteza mechi zake za awali dhidi ya Tottenham Hotspur, Arsenal na Brighton na kama hiyo haitoshi tayari imeanza vibaya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kushindwa kutamba mbele ya Bayern.
“Ni suala la timu na sisi kama timu hatujapata matokeo mazuri, mtu mmoja hawezi kuwapa kiwango cha uchezaji mnachohitaji na si suala la mchezaji mmoja bali ni zaidi ya mmoja akiwamo kocha,” alisema Ten Hag alipoulizwa kuhusu moja ya kosa lililofanywa na kipa wa timu hiyo Onana.
“Hapa tunaangalia wachezaji 11 kufanya kazi yao, tunashambulia na wachezaji 11 na kujilinda na wachezaji 11, kwa hiyo mmoja au wawili wanaposhindwa kufanya kazi yao hapo inakuwa kama umeharibu kila kitu,” alisema Ten Hag.