Paris, Ufaransa
Kiungo wa Paris Saint German (PSG) ya Ufaransa, Idrissa Gueye alikosekana katika mechi ya timu hiyo Jumamosi iliyopita dhidi ya Montpellier jambo ambalo lilionekana ni la kawaida.
Hata hivyo kuna habari kwamba Gueye ambaye pia ni mchezaji wa kimataifa wa Senegal alichukua uamuzi huo akikataa kuvaa jezi yenye nembo ya upinde wa mvua au rainbow ambayo hutumiwa na watetezi wa haki za mashoga, wasagaji na watetezi wa mapenzi ya jinsia moja au LGBT.
Katika mechi hiyo, PSG iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 na tayari vyombo vya habari Ufaransa na Ulaya vimeanza kulifuatilia suala hilo ingawa kocha wake, Mauricio Pochettino alipozungumzia suala hilo alisema Gueye alikosekana kwa sababu binafsi.
Kwa upande mwingine zipo habari kwamba wasimamizi wa soka nchini Ufaransa wamemtaka mchezaji huyo kueleza sababu ni kwanini alikosekana katika mechi hiyo hasa kwa kuwa nembo hiyo ilitumiwa kwenye siku maalum ya kupinga ubaguzi.
Kwenye mitandao ya kijamii mchezaji huyo ameonekana kuwa shujaa akitetewa na watu mbalimbali wakiwamo wachezaji wenzake na katika kundi hilo wamo Ismaila Sarr wa Watford na Cheikhou Kouyate wa Crystal Palace ambao wameunga mkono msimamo wa Gueye wakimtaja kuwa ni shujaa mtu makini mwenye msimamo.
Nyumbani kwao Senegal ambapo mapenzi ya jinsia moja ni jambo lisiloruhusiwa kwa mujibu wa katiba, mchezaji huyo pia ameungwa mkono kila kona kwa msimamo wake, miongoni mwa waliomuunga mkono ni rais wa nchi hiyo, Macky Sall pamoja na wanasiasa na wananchi mbalimbali.
Zaidi ya hilo, Gueye pia anatarajia kuungwa mkono na wamiliki wa PSG ambao ni raia wa Qatar na wanajulikana kwa misimamo yao ya kupinga mapenzi ya jinsia moja huku ikiaminika kwamba huenda msimamo huo ukazidi kumpa umaarufu duniani kote.
Kimataifa Kiungo PSG akataa kuvaa jezi ya kutetea ushoga
Kiungo PSG akataa kuvaa jezi ya kutetea ushoga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
