Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Queens’, Bakari Shime amesema katika mchezo wao dhidi ya Nigeria wataingia kwa tahadhari kubwa kutokana na mbinu nyingi walizonazo wapinzani wao hao.
Timu hizo zitaumana kesho Jumapili kwenye mechi ya marudiano kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia baada ya mechi ya awali iliyoisha kwa sare ya bao 1-1 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Shime alisema hayo Ijumaa hii saa chache kabla ya kuanza mazoezi ya mwisho ya timu hiyo akibainisha kuwa yawezekana Nigeria kuna mbinu zao walizificha, hawakuzitumia kwenye mchezo uliopita, hivyo wanachukua tahadhari juu ya hilo.
“Ni mazoezi ya mwisho ya kutengeneza mipango yetu ya mwisho hapa ugenini, tukiamini tunacheza na timu imara, ngumu na inawezekana walificha baadhi ya vitu tulipokuwa nyumbani na wanaweza kuvionesha hapa kwao, hivyo tunaingia kwa tahadhari kubwa kuhakikisha tunajipanga vizuri kujilinda na kutafuta bao ili tupate faida katika mechi hii,” alisema Shime.
Katika mechi hiyo Tanzanite inahitaji ushindi ili kusonga hatua inayofuata kuelekea michuano hiyo itakayofanyika Colombia, mwakani.
Tanzanite ilitinga hatua hiyo na kukutana na Nigeria baada ya kuifumua Djibouti kwa ushindi wa jumla wa mabao 12-0 baada ya mechi mbili za nyumbani na ugenini zilizopigwa Azam Complex.