Abidjan, Ivory Coast
Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limeanza uchunguzi wa tuhuma za ubaguzi wa rangi kati ya kocha wa Morocco, Walid Regragui na beki wa DR Congo, Chancel Mbemba wanaodaiwa kuzozana hadi kutaka kupigana mara baada ya mechi baina ya timu hizo.
Sambamba na hilo, Caf pia inachunguza madai ya udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na wachezaji wa timu ya Morocco mara baada ya mechi hiyo ya Kundi F katika fainali za Afcon zinazoendelea..
Morocco na DR Congo ziliumana Jumapili iliyopita katika mechi ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1 na baada ya mechi hiyo kuliibuka vita ya maneno baina ya Mbemba na Regragui na kufuatiwa na kutaka kushikana na kutoleana kauli za vitisho.
Taarifa ya Caf iliyotolewa Jumatatu ilithibitisha kuwapo mpango wa kufanyia uchunguzi sakata hilo licha ya Shirikisho la Soka Morocco nalo kuamua kulipooza tukio zima.
Katika tukio hilo, Mbemba na Regragui walilazimika kutenganishwa baada ya kutoleana maneno makali ingawa baadaye kocha huyo alimfuata Mbemba aliyekuwa katika harakati za kufanya maombi kwa lengo la kutaka kumpa mkono.
Mbemba anayeichezea klabu ya Marseille ya Ufaransa alionekana kutokuwa tayari kupeana mkono na kocha huyo akieleza kwamba hakupenda kitendo cha kocha huyo kujaribu kumshawishi mwamuzi kwa kutaka atoe kadi nyekundu.
“Nimeamua kukaa kimya, ni bora, kila mtu ananifahamua mimi, naheshimu kila mtu lakini sikuwahi kuwaza kama ningesikia neno lile kutoka kwa kocha, kwamba neno lile lingetoka mdomoni mwake,” alisema Mbemba.
“Nilimuheshimu kocha lakini video zipo wazi kwenye televisheni, nilitumia muda wangu kumtukuza Mungu,” alisema Mbemba ambaye pia kuna madai kwamba alitolewa kauli za kibaguzi uwanjani hapo na baadaye kupitia mitandao ya kijamii.
Katika taarifa yake, Rais wa Shirikisho la Soka DR Congo (Fecofa), Dieudonne Sambi Nsele-Lutu alisema kwamba kilichofanyika kwa nahodha wao hakikubaliki.
“Haikubaliki kwa nahodha wetu kufanyiwa mashambulizi ya kibaguzi, kutolewa kauli zisizofaa kutoka kwa wachezaji wa Morocco na kocha wao jambo lililoendelea hata wakati tukielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo,” alisema Nsele-Lutu.
Kwa upande wake kocha wa Morocco, Regragui alionekana kushangazwa na madai ya Mbemba kwamba alitoa kauli za ubaguzi wa rangi.
“Anataka kuonesha kwamba kauli yangu ni ya kibaguzi, si uungwana hasa kwa kuwa amezungumza mambo ya dini katika kauli zake, ajaribu kuwa muungwana, nilimpa mkono akaanza kufoka kama mnavyoweza kuona kwenye picha na video zilizopo kila kona,” alisema Regragui.
Morocco leo Jumatano itakamilisha mechi yake ya Kundi F dhidi ya Zambia na ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne wakati DR Congo yenye pointi mbili nayo leo itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kuumana na Tanzania.