Na mwandishi wetu
Winga wa klabu ya Simba, Pape Sakho amepenya kuwania tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuchaguliwa kuwania tuzo ya bao bora kwa msimu huu.
Sakho amechaguliwa kuwania kinyang’anyiro hicho dhidi ya wachezaji wengine tisa wanaoaminika kufunga mabao mazuri msimu huu kupitia ngazi mbalimbali zilizozikutanisha timu za Afrika.
Bao lake lilioingia kwenye tuzo hizo ni lile alilofunga kwa ‘tik-taka’ dhidi ya timu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast walipokutana Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na Simba kushinda kwa mabao 3-1.
Mshambuliaji huyo raia wa Senegal aliyetua Simba msimu huu anakuwa mchezaji wa pili wa Simba kutambulika mchango na kipaji chake CAF baada ya awali shirikisho hilo kumtaja Peter Banda kama miongoni mwa nyota wanne makinda waliofanya vizuri msimu huu kwenye michuano ya ngazi za klabu Afrika.
Sakho tangu atue Simba amekuwa akionesha kiwango kikubwa hasa mwishoni mwa msimu huu akinyakua tuzo mbili za mwezi Juni, Mchezaji Bora wa Simba mwezi Juni na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu mwezi Juni huku akiwa kinara wa asisti msimu huu, akifanya hivyo mara sita.
Hafla ya tuzo hizo za Caf inatarajiwa kufanyika jijini Rabat, Morocco mnamo Julai 21, mwaka huu.
Soka Bao lambeba Sakho CAF
Bao lambeba Sakho CAF
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
