Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumapili imerejea kwenye usukani wa Ligi Kuu NBC baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ikineemeka kwa bao lililofungwa na kinda wake Clement Mzize.
Mzize alifunga bao hilo katika dakika ya 18 ya mchezo huo akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Feisal Salum au Fei Toto na mpira kumshinda kipa wa Kagera, Ismail Kipao ambaye alipishana na mpira huo pamoja na mfungaji aliyeangukia kwenye lango la Kagera.
Yanga pamoja na kupata bao hilo hata hivyo iliponea chupuchupu mara kadhaa kufungwa kutokana na kasi ya wapinzani wao kusaka bao la kusawazisha na kufanikiwa kuutawala mpira kwa muda mrefu wa mchezo huo ambao mara kadhaa uliathiriwa na maji yaliyokuwa katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo na kupunguza kasi kwa kila timu.
Katika dakika ya 68, Kagera walipata penalti baada ya kipa wa Yanga, Djugui Diara kuishika miguu ya Diego Kiiza ambaye alikuwa tayari amempita kipa huyo na kuelekea kupata bao. Hata hivyo mkwaju wa penalti uliopigwa chinichini na Erick Mwijage na kuelekea upande wa kushoto wa Diara uliokolewa na kipa huyo.
Kabla ya hapo katika dakika ya 50, Kagera pia walikosa bao baada ya Anwar Jabir kumuunganishia pasi ya chinichini Mubarak Yusuf ambaye alitakiwa kuugusa kidogo mpira huo ili ujae wavuni lakini alishindwa kuuwahi na mwishowe mpira ulimpita yeye na Diarra na kutoka nje.
Yanga nao katika dakika ya 62 walifanya shambulizi kwenye lango la Kagera kwa mpira ulioanzia kwa Fei Toto ambaye aliunasa mpira wa juu na kuumiliki vizuri kabla ya kumuunganishia Fiston Mayele ambaye naye waliwapunguza mabeki wawili wa Kagera lakini akiwa upande wa kushoto akapiga mpira mkubwa ambao ulitoka nje. Mayele leo mechi ilionekana kuwa ngumu kwake.
Zikiwa zimebaki dakika 10 mpira kumalizika Kagera walilisakama tena lango la Yanga ambapo Mhilu aliinasa pasi ya Kiiza na kufumua shuti la chinichini ambalo lilitoka sentimita chache nje ya lango la Yanga.
Kwa matokeo hayo Yanga sasa imefikisha pointi 23 sawa na Azam ingawa Yanga inaongoza ligi hiyo ikineemeka kwa tofauti ya mabao ya kufunga wakati Azam inashuka katika nafasi ya pili ikifuatiwa na Simba inayoshika nafasi ya tatu.
Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa leo, Mbeya City na Coastal Union zilimaliza mechi yao kwa sare ya mabao 2-2.
Soka Yanga yaizamisha Kagera Sugar
Yanga yaizamisha Kagera Sugar
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
