Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Augustine Okrah amerejea mazoezini baada ya kupona maumivu aliyoyapata katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar iliyomalizika wiki iliyopita.
Daktari wa Yanga, Moses Etutu ameeleza leo Jumatano kuwa mchezaji huyo alishapona tatizo lililokuwa likimsumbua na jana Jumanne alikuwa miongoni mwa wachezaji walioanza mazoezi kujiandaa na mechi za Ligi Kuu NBC na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Okrah alishapona na tayari ameanza mazoezi na timu, ilikuwa ni ajali ya kawaida lakini baada ya kumpatia huduma nzuri na kumpa muda wa kupumzika sasa yupo fiti na ameanza kuitumikia timu yake mpya,” alisema Dokta Etutu.
Alisema mbali na Okrah, wachezaji wengine wote wapo fiti na wanaendelea na maandalizi kambini kwao Avic Town Kigamboni, Dar es Salaam.
Okrah aliyeichezea Simba msimu uliopita, amejiunga na Yanga kwenye dirisha dogo msimu huu akitokea Bencham United ya kwao Ghana.