Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imegawana pointi moja moja na Al Ahly ya Misri baada ya sare ya bao 1-1 katika mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ahly walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 87 mfungaji akiwa Percy Tau aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa baada ya Bakari Nondo Mwamnyeto kuokoa kwa kichwa krosi iliyoelekezwa langoni mwake kabla ya mpira kumkuta mfungaji.
Mwamnyeto alijikuta katika mazingira hayo magumu baada ya Yanga kushambuliwa lakini mpira alioupiga kwa kichwa haukuenda mbali ukawahiwa na Tau ambaye aliujaza wavuni wakati kipa Diarra akiwa mbali kidogo na lango lake.
Baada ya hapo dakika tano ziliongezwa na ndipo Yanga iliponeemeka na muda huo katika dakika ya pili baada ya Pacome Zouazoua kuujaza mpira wavuni kwa shuti kali akiwa amezungukwa na msitu wa mabeki wa Ahly baada ya kuiwahi pasi ya Kennedy Musonda.
Timu zote zilionesha uhai na kujiamini huku zikishindwa kuzitumia nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza, kwa Ahly mchezaji wao tishio, Hussein El Shehata alishindwa kuipatia bao timu yake akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Yanga nayo katika dakika ya 33 ilifanya shambulizi langoni mwa Ahly ambapo Aziz Ki aliuwahi mpira uliombabatiza beki wa Ahly na kupiga shuti la mguu wa kushoto la kimo cha mbuzi lakini mpira ulitoka nje ya lango.
Dakika ya 47, Ahly walifanya shambulizi kali langoni mwa Yanga, shambulizi lililozaa kona tatu ambazo hazikuzaa matunda na dakika nne baadaye Mahmoud Kahraba akiwa karibu na kipa Diarra alishindwa kuipatia Ahly bao.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa, kwanza alimtoa Clement Mzize na kumuingiza Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli akatoka nafasi yake ikachukuliwa na Zawadi Mauya.
Kwa matokeo hayo Yanga inakuwa imezidi kujiweka pagumu kwani hadi sasa ina pointi moja katika mechi mbili wakati Ahly inayoshika usukani katika kundi hilo imefikisha pointi nne katika mechi mbili.
Kimataifa Yanga, Ahly zagawana pointi
Yanga, Ahly zagawana pointi
Read also