Na mwandishi wetu
Timu ya Simba Queens inatarajia kuingia kambini leo Jumatatu kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake 2023/24 unaotarajia kuanza kuunguruma Desemba, mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu na Meneja wa Simba Queens, Seleman Makanya akifafanua kuwa timu yao inaingia kambini kujiandaa na msimu mpya wa ligi hiyo ili kurejesha heshima ya klabu hiyo kwa kuwania ubingwa wa ligi hiyo.
“Tunatarajia kuingia kambini leo na tulikutana na kocha mkuu, Juma Mgunda kwa ajili ya mipango yetu ya msimu ujao na kuona tunaanza kuingia kambini mapema na kuendelea maandalizi ya msimu mpya.
“Bado hatujajua ratiba kwa sababu kesho pia tunatarajia kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuona mchakato wa ratiba tunaanza na nani na wapi,” alisema Makanya.
Alisema msimu huu wamefanya usajili mzuri kwa kuongeza nguvu kwenye mapungufu yaliyojitokeza msimu uliopita na wana uhakika wa kufanya vizuri katika mechi zao kufikia malengo ya kurejesha heshima ya klabu hiyo kutwaa ubingwa.
