Na mwandishi wetu
Straika wa Simba, Jean Baleke amesema wanataka kupunguza machungu ya mechi iliyopita na kujiweka vizuri kuelekea hatua inayofuata kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.
Simba ikiwa ugenini Conakry, Guinea ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa bao 1-0 na Horoya AC.
Kuelekea mechi yao hiyo ya pili itakayopigwa Jumamosi hii kwente Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Baleke alisema anafahamu Raja ni timu nzuri kama wao hivyo watapambana na zaidi wao watakuwa na faida ya kucheza nyumbani.
“Mechi imepita vizuri japo tumefungwa, matokeo ambayo si mazuri lakini tutajitahidi, tutapambana mechi ijayo tupate matokeo yatakayotuweka kwenye timu mbili ambazo zitakwenda hatua inayofuata.
“Kweli Raja ni timu nzuri, kama tulivyo sisi Simba, ni mechi yenye ushindani lakini tutahakikisha tunapata matokeo kwa sababu tutakuwa nyumbani na tunaamini pia matokeo yatakuwa mazuri,” alisema Baleke raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.
Baleke pia alisema kwamba anafurahi kwa mazingira aliyokutana nayo Simba kwani yamekuwa rafiki kwake na amepokewa vizuri na anafurahi kuipambania timu hiyo.
Mchezaji huyo alisajiliwa na Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo la mwezi Januari, mwaka huu na hadi sasa ameifungia mabao mawili kwenye ligi.
