Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kuimarisha kikosi chake cha msimu ujao baada ya leo Jumamosi kumtambulisha winga Luis Miquissone ambaye amerejea katika timu hiyo na kusaini mkataba wa miaka miwili.
Miquissone ambaye habari ya kurejea kwake imezua mjadala siku za hivi karibuni huku baadhi ya wadau wa soka wakiwadhihaki viongozi wa Simba waliojinadi kuhusu kurejea kwa mchezaji huyo.
Mchezaji huyo ambaye tayari amekabidhiwa jezi namba 11, kurejea kwake kunamaliza mabishano ya hivi karibuni yaliyotawala kwenye mitandao ya kijamii.
Miquissone anarejea Simba akiwa mchezaji huru baada ya hivi karibuni kuvunja mkataba na mabingwa wa Afrika, Al Ahly ambayo ilikuwa ikimmiliki tangu msimu wa 2019/20 ilipomnunua kutoka Simba.
Akiwa Ahly hata hivyo Miquissone Septemba mwaka jana aliuzwa kwa mkopo katika klabu ya Abha ya Saudi Arabia ambako pia mambo yake hayakuwa mazuri kabla ya kurejea Simba.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema baada ya kukamilisha usajili wa mchezaji huyo wamesalia na nafasi moja ambayo ni ya kipa na wanatarajia kumtambulisha leo usiku au kesho Jumapili.
“Tumejipanga kuhakikisha msimu ujao Simba inarudisha mataji yake, tumemrudisha Miquissone hakuna asiyejua uwezo wake, imani yetu atasaidia mapambano kuelekea mapambano ya kuirudisha Simba kwenye mafanikio msimu ujao,” alisema Ahmed.
Alisema Miquissone raia wa Msumbiji anatarajiwa kuondoka nchini kuelekea Uturuki kesho kwenda kuungana na wachezaji wenzake kwenye kambi ya maandalizi ya msimu ujao.
Kabla ya kujiunga na Al Ahly, Miquissone aliitumikia Simba kwa misimu miwili na kuipa mafanikio makubwa ikiwemo mataji mawili ya Ligi Kuu NBC.
Miquissone pia aliwahi kutamba na timu za UD Songo ya Msumbiji pamoja na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.