Sao Paulo, Brazil
Mwanasoka gwiji wa zamani wa Brazil, Pele aliyedaiwa kuwa mgonjwa, amewatoa hofu mashabiki akisema kwamba ana nguvu na matumaini makubwa wakati akiendelea na matibabu katika hospitali moja mjini Sao Paulo.
Katika taarifa iliyopatikana jana Jumamosi jioni, Pele alisema kwamba ujumbe mbalimbali wa kumtakia afya njema na baada ya kuangalia mechi ya Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia alisema vyote hivyo vimempa nguvu.
Awali taarifa ya hospitali ilidai kwamba, Pele alikuwa akiendelea na matibabu na hali yake ni nzuri, taarifa iliyokuja baada ya kuwapo habari kwamba hali ya mwanasoka huyo wa zamani ilikuwa mbaya na tiba ya kila mwezi ya saratani ilishindikana.
“Marafiki zangu, nataka kila mmoja awe mtulivu na mwenye matumaini, niko imara na mwenye matumaini makubwa, naendelea na matibabu yangu kama kawaida, ningependa kuwashukuru madaktari wote na manesi kwa kunijali na kunipa matibabu,” ilieleza taarifa hiyo.
“Nina imani kubwa na Mungu na kila ujumbe wa upendo ninaoupokea kutoka kwenu duniani kote, vyote hivyo pamoja na kuiangalia Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia vinaniongezea nguvu! Ahsanteni sana,” ilifafanua taarifa hiyo.
Pele ambaye kwa sasa ana miaka 82 ameshinda Kombe la Dunia mara tatu akiwa na timu ya Brazil, alipelekwa hospitali Jumanne na baada ya kuwapo habari zisizo rasmi kuhusu afya yake, Alhamisi usiku alisema kwamba kwenda kwake hospitali ilikuwa ni tukio la kawaida la kila mwezi.
Salamu za pole zimeendelea kutolewa kutoka maeneo mbalimbali duniani kote kwa kumtakia afya njema gwiji huyo wa soka ambaye aliwahi kufanyiwa operesheni ya kuondolewa uvimbe uliomsababishia maradhi ya saratani.
Kimataifa Pele awatoa hofu mashabiki
Pele awatoa hofu mashabiki
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
