Madrid, Hispania
Mshambuliaji Vinícius Junior ‘Vini Jr’ wa Real Madrid hatimaye amevunja ukimya kwa kukubali ofa mpya inayoandamana na mkataba wa miaka sita itakayomfanya awe na klabu hiyo hadi mwaka 2032.
Klabu ya Real Madrid imethibitisha hilo Alhamisi Agosti 6, 2026 na hivyo kumaliza uvumi wa siku za hivi karibuni kuhusu hatma ya Vini Jr ambaye pia huichezea timu ya taifa ya Brazil.
Mazungumzo baina ya wawakilishi wa Vini na mabosi wa Real Madrid yalikwenda vizuri na inadaiwa kuwa makubaliano yamefikiwa baada ya maslahi ya mchezaji huyo kuboreshwa.
Kabla ya hapo mazungumzo yaliyoanza takriban mwaka mmoja uliopita baina ya pande mbili husika yalikuwa yakikwama na kuibua hofu kuhusu hatma ya Vini Jr na Real Madrid.
Mkataba wa Vini Jr na Real Madrid unafikia ukomo Juni 2027 na kukaibuka habari zilizodai kwamba mchezaji huyo hatoongeza mkataba na tayari alianza kuhusishwa na klabu kadhaa lakini hatimaye amekubali kuongeza mkataba Real Madrid hadi 2032.
“Real Madrid na Vinícius tumekubaliana kuongeza mkataba wa mchezaji wetu, atakuwa katika klabu hii hadi Juni 2032,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.
Vini Jr alijiunga na Real Madrid Julai 2018 wakati huo akiwa na umri wa miaka 18 na katika misimu yake minane na klabu hiyo hadi sasa amebeba mataji mbalimbali.
Awali kulikuwa na habari kuwa Real Madrid ilikuwa tayari kumuuza Vini Jr kama makubaliano yasingefikiwa na moja ya klabu iliyokuwa ikimtaka kwa hali na mali ni Arsenal ya England.
Viní Jr tayari ameshaanza mazoezi katika uwanja wa mazoezi wa Valdebebas unaomilikiwa na Real Madrid baada ya mapumziko.
Mara ya mwisho alionekana akiiwakilisha Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 kabla ya timu hiyo kutolewa na Norway katika hatua ya robo fainali.
