New York, Marekani
Mwaka 1978, mwanasheria Robert Kardashian alifunga ndoa na Kris au Jenner na kupata watoto wanne; Kourtney, Kimberly au Kim, Khloe na Rob. Ndoa hiyo ilivunjika mwaka 1991 na Robert alifariki mwaka 2003.
Robert alipata umaarufu mwaka 1994 na 1995 alipomtetea, O.J Simpson hadi kushinda kesi ya mauaji iliyokuwa mjadala sehemu mbalimbali duniani. Simpson, Mmarekani mwenye asili ya Afrika alidaiwa kumuua aliyekuwa mkewe, Nicole Brown ambaye ni mzungu miaka miwili baada ya kutalikiana.
Leo hii ukiizungumzia familia ya Kardashian huhitaji tena kumtaja Robert, utawazungumzia wanadada warembo wafanyabiashara matajiri ambao wameutumia vizuri urembo wao kupiga pesa kupitia uanamitindo, mauzo na maonyesho ya mavazi, vipindi vya televisheni hadi kutoa kitabu cha Kardashian Konfidential cha mwaka 2010.
Kourtney (42)
Kourtney ni mwanamitindo na mshiriki wa vipindi vya televisheni akishiriki kipindi maarufu cha familia hiyo cha Keeping Up with Kardashians na vipindi vingine vya Kourtney and Khloe Take Miami na Kourtney and Kim Take New York ambavyo ni kama mwendelezo wa Keeping Up with Kardashians.
Kourtney na ndugu zake pia wamekuwa wakiuza mavazi ya aina mbalimbali pamoja na manukato huku wakinufaika kupitia mitandao ya Facebook, Twitter na Instagram kwa kujiingizia pesa kwa kila ‘post’. Kourtney aliwahi kutajwa kupata dola 75,000 hadi 200,000 kupitia mitandao ya Facebook na Twitter.
Kwenye mahusiano, Kourtney aliwahi kuwa mpenzi wa Scott Disick kati ya mwaka 2005 hadi 2015 na a kupata watoto watatu, baada ya hapo akawa na mwanamitindo, Younes Bendjima kati ya mwaka 2017 na 2018.
Mapema mwaka huu zimekuwapo habari kwamba Kourtney anatoka na mwanamuziki Travis Barker na wawili hao inadaiwa huenda wakafunga ndoa wakati wowote.

Kim (40)
Kama dada yake Kourtney, Kim alianza kupata umaarufu akiwa rafiki wa mwanamitindo Paris Hilton, baadaye akawa gumzo zaidi baada ya mkanda wake wa ngono na aliyekuwa mpenzi wake, Ray J kuzagaa mitandaoni mwaka 2007. Ni wakati huo huo alishiriki vizuri na kukipa umaarufu zaidi kipindi cha Keeping Up with Kardashians.
Kwa warembo wa familia ya Kardashian, Kim amepiga pesa za maana, mbali na vipindi vya televisheni ana biashara za mavazi na manukato na mwaka 2017 alianzisha kampuni za biashara ya urembo, mitindo na manukato za KKW Beauty na KKW Fragrance hiyo ni mbali na mamilioni ya wafuasi wanaomfuatiia kwenye mitandao hasa ya Twitter na Instagram na kumfanya alipwe fedha kibao.
Mwaka 2015 jarida la Time, lilimtaja katika orodha ya wanawake 100 maarufu huku akitajwa kuwa mshiriki wa kwenye vipindi vya televisheni mwenye malipo makubwa akidaiwa katika mwaka huo pato lake lilifikia Dola 53 milioni.
Kim alifunga ndoa mwaka 2000 na Damon Thomas, msanii wa R&B lakini ndoa ilivunjika mwaka 2004, mwaka 2011 akaolewa na Kris Humphries nyota wa mpira wa kikapu katika ligi ya NBA, Marekani lakini ndoa hiyo ilivunjika mwaka 2013 huku ikidaiwa kuwa ndoa hiyo ilikuwa ni mpango maalum wa Kim kujiongezea umaarufu na kujiimarisha zaidi kibiashara ingawa Kim alipinga.
Mwaka 2014 akaangukia kwa rapa Kanye West, ndoa iliyokuwa maarufu kwa namna vyombo vya habari vilivyokuwa vikiwakifuatiliwa kila kona huku Kim akiitwa kwa jina la Kim Kardashian West. Kim na Kanye wana watoto wanne lakini Septemba mwaka huu ndoa yao kama ile ya Kourtney nayo iliota mbawa.

Khloe (37)
Ni mrembo aliyefuata nyayo za dada zake, kwenye mitindo yumo na hajajiweka kando kwenye televisheni, ushiriki wake katika Keeping Up with Kardashians unachangia kumuweka juu.
Mwaka 2016 alijiongeza zaidi kwa kuanzisha kipindi cha televisheni cha Kocktails with Khloe pamoja na kipindi kingine cha mambo ya afya na mazoezi cha Revenge Body with Khloé Kardashian.
Khloe, pia anafanya biashara ya manukato, mwaka 2011 yeye na aliyekuwa mumewe walitangaza kuuza manukato ya wanawake na wanaume waliyoyapa jina la Unbreakable na mwaka 2012 wakaja na manukato mengine waliyoyapa jina la Unbreakable Joy.
Mwaka 2008, Khloe alitajwa kuwa katika mapenzi na nyota wa mpira wa kikapu wa klabu ya Los Angeles Lakers, Rashad McCants lakini miezi saba baadaye walitengana na akahamia kwa nyota mwingine wa kikapu, Lamar Odom waliyefunga naye ndoa Septemba 2009 na Khloe kuitwa Khloe Kardashian Odom lakini ndoa hiyo nayo iliota mbawa mwaka 2016.
Rob (34)
Kaka pekee mwenye dada watatu, hajajiweka nyuma katika kusafiria nyota ya dada zake, Rob ni mshiriki mzuri wa Keeping Up with Kardashians, jina lake lilikuwa mjadala mitandaoni mwaka 2016 alipoanza mahusiano ya kimapenzi na mwanamitindo, Blac Chyna na kupata mtoto wa kike waliyempa jina la Dreem Renee aliyezaliwa Novemba 2016, lakini mwezi mmoja tu baada Dreem kuzaliwa wawili hao waliachana.
Rob pia ana dada wengine wawili, Kendall na Kylie ambao ni wa baba mwingine, nao wamefuata nyayo za Kardashian Family kwa kuutumia urembo kupiga pesa.

Kendall Jenner (26)
Kendall ni mwanamitindo, mfanyabiashara na mshiriki mzuri wa vipindi vya televisheni, alianza kupata umaarufu kupitia Keeping Up with the Kardashians na kwenye maonyesho ya mitindo ya Paris, Milan na New York.
Mwaka 2017 jarida la Forbes lilimtaja Kendall kuwa ni mwanamitindo anayelipwa fedha nyingi zaidi akimpiku, Gisele Bündchen ambaye amekuwa akitamba kwa zaidi ya miaka 10. Kendall kwa sasa yuko katika mahusiano ya kimapenzi na nyota wa mpira wa kikapu wa NBA, Devin Booker.

Kylie Jenner (24)
Ni mwanamitindo, mfanyabiashara na mshiriki wa vipindi vya televisheni, alipata umaarufu kupitia kipindi cha E! reality ambacho ni sehemu ya Keeping Up with the Kardashians, pia ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya vipodozi ya Kylie Cosmetics, anatajwa kuwa mwanamke mwenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram akiwa na umri mdogo.
Katika mauzo ya mavazi ameshirikiana vyema na dada yake kupitia kampuni yao ya Kendall & Kylie na mwaka 2015 alizindua aina ya vipozozi vyake alivyovipa jina la Kylie Lip Kits na baadaye kubadili jina hilo na kuwa Kylie Cosmetics.
Kati ya mwaka 2014 na 2015, jarida la Time lilimtaja yeye na Kendall kuwa ni wasichana wa umri mdogo maarufu duniani kwa kuangalia nguvu yao kwenye mitandao ya kijamii.
Mwaka 2019 Forbes lilimtaja Kylie kuwa na pato linalofikia dola bilioni 1 na kumfanya awe msichana aliyepambana kufikia hadhi ya ubilionea akiwa mdogo, wakati huo alikuwa na miaka 21.
Hata hivyo hoja ya kwamba amepambana hadi kuwa bilionea imekuwa ikipingwa na wale wanaoamini kuwa utajiri wake umebebwa na umaarufu wa familia huku akilaumiwa kuwa japo ni tajiri mwenye pesa lakini baadhi ya taarifa zake zinakuzwa ili kumpaisha zaidi.
KKylie aliwahi kuwa mpenzi wa rapa Tyga yaani mpenzi wa zamani wa Blac ambaye pia alikuwa mpenzi wa Rob, kaka yake Kylie, aliwahi kuonekana kwenye video za nyimbo za Tyga za Stimulated na aka Dope’d Uppen.
Kuanzia mwaka 2017, Kylie amekuwa akionekana na mwanamuziki Travis Scott na alionekana katika video ya wimbo wa Scott wa Stop Trying to Be God na hadi sasa wana mtoto mmoja wa kike aitwaye, Stormi Webster.
