Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG) ya Ufransa, Kylian Mbappe huenda akaikosa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich baada ya kuumia jana Jumatano katika mechi ya Ligi 1 dhidi ya Montpellier.
Mbappe ambaye awali katika mechi hiyo alikosa penalti mara mbili, aliumia goti na misuli ya paja wakati akikabiliana na kiungo wa Montpellier, Leo Leroy na kutolewa dakika ya 21 ingawa timu yake ilitoka na ushindi wa mabao 3-1.
Sura ya kinyonge ya mchezaji huyo wakati akitoka uwanjani vilitosha kuibua hofu kwamba kulikuwa na tatizo kwa mshambuliaji huyo ambaye pia huichezea timu ya Taifa ya Ufaransa.
Haikuweza kufahamika mara moja ukubwa wa majeraha aliyoyapata lakini mazingira ya tukio zima kuanzia kutolewa nje mapema na unyonge aliouonyesha vilitosha kutoa picha kwamba huenda tatizo si dogo licha ya kocha wake Christophe Galtier kujipa matumaini.
“Ni michubuko au kugongana? Bado kwa sasa hatuna uhakika lakini halionekani kuwa tatizo kubwa, hatuna wasiwasi wowote,” alisema kocha Galtier.
Mbappe alitarajia kufanyiwa vipimo leo Alhamisi wakati ili kujua ukubwa wa tatizo ingawa zikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya kuumana na Bayern katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, uwezekano wa mshambuliaji huyo kuwa fiti unatiliwa shaka.
Kinachoonekana kuwa wazi kwa sasa ni kwamba Mbappe ataikosa mechi ya Februari 8 ya Kombe la Ufaransa dhidi ya Marseille na kisha ataikosa mechi ya Ligi 1 ya Februari 11 dhidi ya Monaco huku majaliwa ya mechi na Bayern nayo yakiwa njia panda.
Ukiachana na Mbape wachezaji wengine majeruhi wa PSG ni Sergio Ramos ambaye pia alilazimika kutoka mapema katika mechi ya Jumatano wakati Neymar naye bado anasumbuliwa na enka na hakuwapo kwenye mechi na Montpellier.
