Doha, Qatar
Kocha wa timu ya England, Gareth Southgate amesema atafanya tathmini na Chama cha Soka (FA) baada ya England kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya robo fainali kabla kuamua hatma yake.
Southgate mwenye umri wa miaka 52, alikabidhiwa kwa mara ya kwanza majukumu ya kukinoa kikosi cha England mwaka 2016 lakini ana mkataba ambao unafikia ukomo baada ya fainali za Ulaya za mwaka 2024 au Euro 2024.
Baada ya England kupoteza mechi ya robo fainali mbele ya Ufaransa jana kwa kuchapwa mabao 2-1, Southgate alisema: “Haya mashindano yanakuchukulia muda mwingi, na nahitaji kufanya tafakari, huwa tunafanya hivyo kila baada ya mashindano na hilo ni jambo sahihi kulifanya.”
Wachezaji wa zamani wa England, Gary Neville na Ian Wright pamoja na nahodha wa zamani wa Jamhuri ya Ireland, Roy Keane kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakisema kwamba wangependa kuona Southgate akiendelea na kazi hiyo.
Baada ya kuifikisha England hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Ufaransa, pamoja na hatua ya fainali kwenye Euro 2020, Southgate ameshindwa kuifikisha tena England kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia baada ya kushindwa kutamba mbele ya Ufaransa.
“Najivunia kile ambacho wachezaji wangu wamekifanya, si tu jioni hii (jana) bali kwa kipindi chote cha michuano hii, nafikiri timu imepiga hatua mbele katika maeneo yote,” alisema Southgate kocha wa zamani wa timu ya vijana chini ya miaka 21 ya England.
Katika mechi hiyo, nahodha wa England, Harry Kane aliisawazishia England bao kwa mkwaju wa penalti na kufanya matokeo yawe sare ya bao 1-1 lakini Olivier Giroud aliifungia Ufaransa bao la pili na baadaye England ikapata penalti ambayo Kane alishindwa kuitumia vizuri kuipatia England bao la kusawazisha.
LigiKuu Southgate ajifanyia tathmini England
Southgate ajifanyia tathmini England
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
