Berlin, Ujerumani
Kiungo wa zamani wa Real Madrid, Arsenal na timu ya Taifa ya Ujerumani, Mesut Ozil ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 34.
Ozil ambaye ni Mjerumani mwenye asili ya Uturuki, ameichezea timu ya Taifa ya Ujerumani mara 92 na kubeba Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil akiwa na timu hiyo.
Katika soka la klabu, Ozil amebeba mataji manane yakiwamo manne ya FA na moja la La Liga alilobeba mwaka 2012 akiwa na Real Madrid.
“Ni safari ya aina yake iliyojaa matukio yasiyosahaulika na yenye kuvutia, nina heshima ya kipekee kuwa mchezaji profesheno kwa miaka takriban 17 na najiona mwenye kushukuru kwa fursa hiyo,” alisema Ozil kupitia mitandao ya kijamii.
“Lakini katika wiki na miezi ya karibuni pia nimekuwa nikipata majeraha na ikaonekana wazi kabisa kwamba ni wakati wa kuachana na hatua hii kubwa niliyofikia kwenye soka,” aliongeza Ozil.
Kabla ya kujiunga na Real Madrid mwaka 2010 hadi 2013 na Arsenal kuanzia 2013 hadi 2021, Ozil alizichezea klabu za Schalke 04 na Werder Bremen za Ujerumani.
Baada ya kutoka Arsenal alijiunga na Fenerbahce ya Uturuki aliyoichezea kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 na baada ya hapo alijiunga na Istanbul Basaksehir pia ya Uturuki na ndipo alipostaafia.