Na mwandishi wetu
Bondia Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ amemtaka mpinzani wake Banja Hamisi kuwa makini kwani amepanga kumpiga kwa sifa ili adhihirishe ni namna gani alikuwa akijipanga vilivyo kuelekea pambano hilo.
Dulla atapanda ulingoni kupambana na Banja katika pambano la awali kabla ya pambano la ‘main card’ litakalowakutanisha Ibrahim Mgenda ‘Class’ dhidi ya Khamis Muathai Agosti 27, mwaka huu visiwani Zanzibar.
“Banja nakuja Zanzibar huko, jiandae vizuri usije ukakimbia. Kuna ngumi za mikiki anapigana Mandonga (Karim), kuna ngumi za burudani anazo Ibra Class ila mimi napiga ngumi za sifa, sababu nafanya mazoezi ya sifa, lazima mtu apigwe nia yangu ni kuonesha umwamba wangu upya,” alisema Dulla.
Mbali ya mapambano hayo yatakayopigwa kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, pia kutakuwa na pambano lingine la utangulizi la Mandonga dhidi ya Muller Junior.
Pambano hilo lililoandaliwa na Tosh Sports kupitia Kampuni ya Tosh Cargo, linatarajiwa kuwa la kwanza kufanyika Zanzibar tangu kuruhusiwa kwa mchezo huo visiwani humo.