Na mwandishi wetu
Wapinzani wa Simba katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri hatimaye wametua nchini Jumatano hii wakiwa kamili tayari kwa mechi hiyo itakayopigwa Ijumaa.
Msafara wa wachezaji na viongozi wa timu hiyo ulionekana Jumatano hii mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) huku wakiwa na mabegi makubwa na mizigo mingine iliyokuwa ikisukumwa kwa vitoroli vya JNIA.
Mazingira ya timu hiyo yalitoa picha ya kile kilichokuwa kikijadiliwa na kuzungumzwa kwa siku za karibuni kwamba wakiwa Tanzania, wachezaji wa Ahly watajikimu kadri wawezavyo kwa kila kitu kuanzia vyakula na mahitaji mengineyo ya msingi.
Simba na Ahly zitaoneshana ubabe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam hiyo ikiwa ni mechi ya kwanza kabla ya kurudiana baadaye mjini Cairo Misri ambapo mshindi atakuwa amejikatia tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.
Ahly kwa sasa ndio mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, michuano ambayo ni mikubwa na yenye hadhi ya juu kwa ngazi ya klabu barani Afrika na watacheza na Simba wakiwa na dhamira ya kulitetea taji hilo.
Simba kwa upande wao watapenda kuitumia mechi hiyo kwa lengo la kupata ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri katika mechi ya marudiano ili waweze kuweka historia kwa kumtoa bingwa mtetezi na kujikatia tiketi ya nusu fainali.
Kimataifa Ahly watua Dar wakiwa kamili
Ahly watua Dar wakiwa kamili
Read also
