Na mwandishi wetu
Kuelekea mechi ya kesho ya hatua ya mtoano kuwania kufuzu kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao, timu ya Tanzania Prisons imejinasibu kuwa itahakikisha inamaliza kila kitu kwenye mchezo wao huo wa awali dhidi ya Mtibwa Sugar.
Prisons itakuwa nyumbani kwenye mechi hiyo Uwanja wa Sokoine, Mbeya kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Julai 6, mwaka huu Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Kocha msaidizi wa Prisons, Shaban Mtupa ameeleza jinsi gani wanahitaji matokeo ya mabao ya kutosha kwenye mechi hiyo ili kupata uhakika wa matokeo mazuri kuelekea mechi ya marudiano na mwisho wacheze tena Ligi Kuu msimu ujao.
“Mchezo hautakuwa mwepesi, ni mechi inayohitaji tupate matokeo mapema tukiwa nyumbani, ushindi mnono utakaotuweka kwenye mazingira mazuri kuelekea marudiano. Tumeshakubaliana na wachezaji na benchi la ufundi kwamba kesho tunahitaji ushindi.
“Unajua Mtibwa si timu nyepesi lakini sisi pia tunahitaji kusalia kwenye ligi, hatuhitaji tena kibarua cha kwenda kucheza mchezo mwingine na JKT (Tanzania), hivyo tutahakikisha tunamaliza hii kazi mapema,” alisema Mtupa.
Upande wa Mtibwa, ofisa habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru alikiri kuwa na vita nzito mbele yao dhidi ya Prisons lakini uimara wa kiafya wa wachezaji wao imekuwa taarifa nzuri kwa benchi lao la ufundi katika kuipambania nafasi hiyo.
“Tumefika Mbeya siku ya tatu leo yote tukihitaji kukaa sawa mapema kwenye kila eneo, vita hii ni kubwa si nyepesi hata kidogo lakini maandalizi yetu nayo yamekuwa mazuri na ripoti zinaonesha hakuna mchezaji tutakayemkosa kwa majeruhi, hivyo inawapa uhakika benchi la ufundi katika matumizi ya kikosi kitakachopambana kesho,” alisema Kifaru.
Timu hizo zinacheza mechi hiyo baada ya Mtibwa kumaliza nafasi ya 13 kwa pointi 31 na Prisons wa 14 kwa pointi 29 hivyo wanapambania ushindi wa mechi hizo mbili ili moja isalie Ligi Kuu.
Itakayofungwa hapo, itapepetana na JKT Tanzania katika mechi mbili zitakazopigwa Julai 9 na 13, mwaka huu kuitafuta timu nyingine itakayoungana na mshindi wa mechi za awali kukamilisha idadi ya timu 16 za Ligi Kuu msimu ujao.
Soka Prisons yajigamba kuimaliza Mtibwa
Prisons yajigamba kuimaliza Mtibwa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
