Na mwandishi wetu
Bondia Mtanzania, Selemani Kidunda (pichani) amesema maandalizi kuelekea pambano lake dhidi ya Asemahle Wellem wa Afrika Kusini yamekamilika na amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpa sapoti.
Pambano hilo la uzito wa superwelter litakalokuwa na raundi 12 limepangwa kufanyika Machi Mosi, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Warehouse, Dar es Salaam.
Kidunda alisema maandalizi aliyoyafanya na kujua vizuri mbinu za mpinzani wake vinampa matumaini ya kushinda pambano hilo linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
“Nataka kuubakiza nchini mkanda wa WBF, hata mashabiki zangu wanapenda kuona hilo na mimi nitahakikisha siwaangushi kwa kushinda kwa pointi za kutosha na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania,” alisema Kidunda.
Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 10, saba kati ya hayo akishinda kwa KO, alisema ushindi wake katika pambano hilo utakuwa ni salamu tosha kwa mabondia wengine ambao wanatamani kucheza naye.