Doha, Qatar
Kocha wa Morocco, Walid Regragui amesema kwamba Morocco ni moja ya timu nne bora duniani kwa sasa wakati wakiwa katika mpango wa kuweka historia nyingine wakipigania kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Dunia.
“Kwa nini tusifikie hatua ya fainali ya Kombe la Dunia, tutaonyesha hamasa kubwa, tutawashangaza, tumekuja katika mashindano haya kubadili mtazamo kuhusu bara letu,” alisema Regragui.
“Kabla ya kila mechi watu walikuwa wakifikiria tunatolewa lakini hadi sasa tuko hapa, tunaikaribia ndoto yetu na tutapambana kuifikia,” aliongeza kocha huyo ambaye alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo, Agosti mwaka huu na aliwahi kunukuliwa akisema kwamba wanawaza kubeba Kombe la Dunia.
“Kama tunasema nusu fainali imetosha, hilo sikubaliani nalo, hatujatosheka na nusu fainali au hata kuwa timu ya kwanza Afrika kufikia hatua hiyo, tunataka kwenda mbele zaidi, unaweza kudhani huo ni ukichaa lakini ukiwa na ukichaa kidogo hilo ni jambo zuri,” alisema.
Morocco kesho Jumatano inacheza na Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi katika mechi ya nusu fainali, mechi ambayo inaifanya timu hiyo kuwa ya kwanza Afrika kufikia hatua hiyo.
Kabla ya Morocco, timu pekee za Afrika zilizokuwa na rekodi nzuri kwenye Kombe la Dunia ni Senegal, Ghana na Cameroon ambazo zilifikia hatua ya robo fainali.
Kimataifa Kocha Morocco ana mzuka wa kombe
Kocha Morocco ana mzuka wa kombe
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
