Na mwandishi wetu
Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya Yanga kurudiana na Rivers United katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema jeshi lao lipo tayari kwa mchezo huo.
Yanga itashuka kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam Jumapili hii kukamilisha mechi hiyo ya mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali huku ikiwa tayari imetanguliza mguu mmoja mbele kufuatia ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa awali uliochezwa Nigeria wiki iliyopita.
Kaze ameeleza kuwa maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na wameupa uzito mkubwa mchezo huo licha ya kwamba wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele hatua inayofuata.
“Hatuwezi kuidharau Rivers United kwa ushindi ambao tumeupata kwao hata wao wanaweza kufanya hivyo ndio maana tunawasisitiza wachezaji wetu kuongeza umakini na kucheza kwa kujituma sababu bado hatujafuzu nusu fainali,” alisema Kaze.
Kocha huyo ameeleza kuwa wamepanga kucheza kama walivyofanya kwenye mechi za hatua ya makundi walizocheza nyumbani lengo ni kupata mabao ya mapema yatakayowahakikishia safari ya nusu fainali.
Upande wa pili, wapinzani hao wa Yanga, Rivers United wanatarajiwa kuwasili nchini usiku wa kuamkia kesho wakitokea kwao Nigeria.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema wakiwa kama wenyeji, wamewaandalia wageni wao mazingira mazuri ikiwemo usafiri na hoteli nzuri ili wakiwafunga wakose visingizio.
Yanga inahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga mbele hatua inayofuata ya nusu fainali na kuweka historia ya kufika hatua hiyo.