Istanbul, Uturuki
Mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema na kocha wake Carlo Ancelotti wametwaa tuzo za mchezaji bora na kocha bora wa mwaka wa Uefa.
Kwa Benzema tuzo hiyo inakuwa na maana kubwa kwani inazidi kudhihirisha kile ambacho kinatajwa na wengi kwamba mchezaji huyo ndiye atakayeibuka kinara wa Ballon d’Or akiwa amebebwa na mafanikio mengi moja kubwa ni kuiwezesha Real Madrid kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa msimu ulioipita, Benzema ameiwezesha Real Madrid kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la La Liga na hapo hapo akionyesha uwezo wake kwa kupiga hat trick mbili katika mechi dhidi ya Chelsea na Paris Saint Germain.
Tuzo ya mchezaji bora na kocha bora wa Uefa zinatolewa Alhamisi hii jijini Istanbul, Uturuki ambapo pamoja na mambo mengine ratiba na makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msmu wa 2022/23 ilitarajiwa kutolewa.
Kwa upande wa Ancelotti yeye alitwaa tuzo ya kocha bora akiwabwaga makocha wenzake, Jurgen Klopp wa Liverpool na Pep Guardiola wa Man City.
Alipoulizwa ni vipi ameweza kuwa kocha mwenye mafanikio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ancelotti alisema, “Ni mapenzi niliyonayo katika mchezo huu na ubora wa wachezaji nilionao, msimu uliopita tulikuwa na muunganiko wa aina yake kati ya wachezaji wakongwe na vijana, mchanganyiko ulikuwa mzuri pamoja na mashabiki ambao wametusaidia kupata mafankio ambayo huwezi kuamini.”
Akimzungumzia Benzema Ancelotti alisema, “Karim si tu ni mshambuliaji mzuri na mwenye mabao mengi bali pia ni mwanasoka wa aina yake anayebebwa na tabia na mienendo yake siku hadi siku.”
Benzema yeye aliwabwaga kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois na Kevin De Bruyne wa Man City hadi kutwaa tuzo hiyo ambayo jopo la wanaochagua mshindi lilikuwa na wawakilishi wa klabu na wanahabari ambao walikuwa na jukumu la kuchagua katika kundi la wachezaji 15 waliopendekezwa na kutokana na utafiti wa jopo la kamati ya ufundi ya Uefa.
Mwaka 2021, Benzema alishika nafasi ya nne katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or akiwa nyuma ya Lionel Messi, Robert Lewandowski na Jorginho lakini safari hii wakati tuzo zikisubiriwa kutolewa Oktoba mwaka huu jina lake limekuwa likitajwa zaidi kuliko wachezaji wengine.
Kimataifa Benzema, Ancelotti watwaa tuzo Uefa
Benzema, Ancelotti watwaa tuzo Uefa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
