Cairo, Misri
Wakati Morocco ikitangazwa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Matafa ya Afrika (Afcon) 2025, nchi majirani Afrika Mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda zimeshinda nafasi ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo mwaka 2027.
Akitangaza ushindi wa nchi hizo, leo Jumatano Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe alisema kwamba fainali za 2027 zitakuwa nzuri kutokana na namna ambavyo marais watatu wa nchi za Afrika Mashariki walivyojitoa kwa jili ya fainali hizo.
“Hii inaonesha ni kwa kiasi gani ukanda huu ulikuwa na shauku kubwa ya kuwa wenyeji wa fainali hizi,” alisema Motsepe mara baada ya mkutano wa CAF uliofanyika mjini Cairo.
Tanzania, Kenya na Uganda zimeshinda nafasi hiyo dhidi ya nchi za Senegal, Botswana na Algeria ambayo inadaiwa iliamua kujitoa siku mbili kabla ya kutangazwa kwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho.
Kufuzu kwa nchi hizo za Afrika Mashariki ni hatua ya kwanza lakini bado nchi hizo zina kazi ya kuweka miundombinu hasa ya viwanja katika ubora ambao wakaguzi wa CAF watauridhia.