Na Jonathan Haule
Katika Filamu ya Huba, Happy, kama lilivyo jina lake ameanza kufurahia huba la JB baada ya kujawa hofu siku za mwanzo, hapo hapo Tesa mwanamke jasiri anayeamini kuwa ndiye mwenye hadhi ya kuwa na JB akiteseka kama lilivyo jina lake baada ya kuachwa…
Ilipofika Filamu ya Huba juma hili ni mwendelezo wa visa vyenye utata katika mahaba miongoni mwa wahusika wa filamu hii ambao kwa kiasi kikubwa wameendelea kudhihirisha namna wanavyofanikisha kufikisha ujumbe wa visa hivyo kama lilivyo jina la filamu yenyewe.
Wakati Happy akianza kufurahia huba na utajiri wa JB, Tesa anajikuta akiwa mnyonge, anapoteza ujasiri na ubabe wote aliojipamba nao katika filamu hii, chozi linamtoka, anajawa hasira, hatimaye anamalizia hasira zake kwa Mzee Mwinyi na mkewe ambao amewapa hifadhi nyumbani kwake, anawafokea kwa makosa yasiyoeleweka, na kama hiyo haitoshi anaamua kuwatimua akiwataka warudi kijijini.
Happy kwa upande wake ameanza kuonjeshwa jeuri ya pesa za JB, amewekewa watu maalum wa kumpa mavazi ya uhakika ili kumfanya afanane na mwanamke mwenye kuishi maisha ya kifahari, awe na hadhi ya mpenzi wa tajiri JB.
JB hajawa nyuma katika kuonyesha jeuri ya pesa, hataki Happy tena atumie usafiri mwingine zaidi ya usafiri wa hadhi, apelekwe anakotaka na dereva au JB ampeleke mwenyewe. Zaidi ya hilo JB pia anajipanga kwenda naye Dodoma katika shughuli zake za kibiashara.
Tesa hajakubaliana na kinachoendelea kati ya Happy na JB, anaamua kumshirikisha Nicole ambaye kama Tesa naye ameporwa JB, ni wanawake wawili wanaougulia maumivu ya kuporwa bwana, wanajipanga kuunganisha nguvu dhidi ya Happy, msichana ambaye Nicole ndiye aliyemuongoza katika mambo yote ya ukahaba lakini akafikia hatua ya kumpiku kwa JB, tajiri mpenda totoz.
Kuungana kwa Nicole na Tesa ni tukio mojawapo linalomfanya mfuatiliaji wa filamu hii kusubiri kwa hamu kuanzia Jumatatu hii na kuendelea ili kujua nini kitatokea kati ya Tesa na Nicole dhidi ya Happy, na nini atakifanya JB iwapo Nicole na Tesa wataamua kuunganisha nguvu na kumkabili Happy? Na je ni mbinu gani watakayokuja nayo Nicole na Tesa dhidi ya Happy?
Hapo hapo kila mtu atapenda kujua nini hatma ya Happy na Chidi, wapenzi wawili ambao licha ya umaskini wao lakini walikuwa na huba lisilotia shaka kabla Happy hajaingia katika ukahaba na kuangukia kwa JB na taratibu ameanza kumsahau Chidi, mtu wake ambaye awali alikuwa akimuulizia mara kwa mara.
Vipi mpango wa Chidi kutoroka kwenye kambi anakofanya shughuli za kilimo, mpango ambao tayari umevurugwa na Carlos licha ya awali kulipigania suala la kutoroka na kumshirikisha Chidi, lakini kubwa linalomtesa Chidi ni pale zinapomjia kumbukumbu za Happy.
Mwanamama mwingine jeuri na mwenye pesa zake, Kibibi hatimaye anaelekea kusalimu amri kwa Devi licha ya ukali na maneno ya kijeuri aliyokuwa akimtolea wakati Devi akijaribu kurudisha penzi lao la zamani, awali hakukuwa na dalili zozote za Kibibi kumkubali Devi lakini taratibu ameanza kulegea, ama kweli penzi halina jemedari, anamlilia Devi na kumueleza matatizo yaliyomkuta.
Walipofikia Devi na Kibibi ni vigumu kuamini kwamba ni Kibibi huyu huyu aliyekuwa akimuangalia Devi kwa jicho la dharau na kumsikiliza kwa namna ya kutojali nini anasema, kumlaza sebuleni kwenye kochi lakini sasa kinachoonekana ni kama vile ile hadithi ya hakuna mkate mgumu mbele ya chai taratibu inaanza kujidhihirisha. Kuanzia Jumatatu bila shaka tutaona mengi ya wawili hawa. Je Kibibi ataanza kumbadilikia Devi au Devi ataendelea kumtuliza kama ambavyo tayari kafanikiwa kumtuliza?
Nelly, mtoto pekee wa JB naye ni kama amechanganywa kwa kitendo cha baba yake kuingia katika mahusiano na Happy, anajaribu kumdodosa Happy lakini kabla hajafika mbali anakubali ukweli ambao haupendi na haumfurahishi kwamba baba yake haoni hasikii kwa Happy na hivyo kwake hana ujanja zaidi ya kukubali kwamba Happy sasa anakuwa kama mama yake.
Mfungwa Judi pamoja na kuwa jela lakini akili yake bado haijatoka kwa Tima, haachi kumuwaza mara kwa mara licha ya kwamba Tima hana mpango naye, katika matukio ya wawili hao Judi anajawa hasira kwa anachojua kwamba Tima ametoa mimba yake na hivyo anaamua kumfanyia visa vya kila aina huku akiendelea kutumikia kifungo gerezani.
Tima hakubaliani na Judi, anapinga hoja ya kutoa mimba, anaamua kumfuata jela na hapo hapo inatokea tafrani baina ya wawili hao, Judi akishikilia msimamo wake kwamba Tima ametoa mimba yake.
Mbali na kuvurugwa na Judi, Tima pia hana amani baada ya penzi lake na Devi kusambaratika licha ya matumaini makubwa aliyokuwa nayo kwa Devi hasa baada ya Judi kufungwa na Devi kutibuana na Kibibi na hivyo Tima akawa kimbilio pekee la Dvi.
Devi anayepigiwa hesabu na Tima kwa sasa kitu pekee anachofanya ni kupigania kulirudisha penzi lake kwa Kibibi jambo ambalo tayari ameanza kulifanikisha na hivyo nafasi ya Tima haipo.
Visa hivyo na vinginevyo vingi vikiwamo vya kishirikina vinavyohusisha mambo ya mahaba ni kati ya matukio yanayoipamba Filamu ya Huba. Tukutane juma lijalo kwa muendelezo wa uchambuzi wa filamu hii iliyojaa visa vya kusisimua…
BongoMovie Happy afurahia huba la JB, Tesa ateseka
Happy afurahia huba la JB, Tesa ateseka
Related posts
Read also
