Leverkusen, Ujerumani
Klabu ya Bayer Leverkusen hatimaye imebeba kwa mara ya kwanza taji la Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 mbele ya Werder Bremen.
Ushindi huo mnono uliopatikana katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili hii unaifanya timu hiyo kuweka rekodi si tu ya kulibeba taji hilo kwa mara ya kwanza bali pia imefanya hivyo ikiwa na mechi tano mkononi.
Bayer chini ya kocha Xabi Alonso katika mafanikio hayo pia wameweka rekodi ya kuwa timu ambayo haijapoteza hata mchezo mmoja msimu huu katika mashindano yote hadi sasa.
“Tunajisikia furaha, nadhani hii si kwa upande wetu tu bali pia ni kwa watu wengine wengi ambao wamekuwa wakiisaka ndoto hii kwa miaka mingi,” alisema Alonso.
Alonso pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza makocha waliopita wa klabu hiyo akisema nao wana mchango katika mafanikio hayo na kufafanua kwamba kitu chochote kinapokuwa kimefanywa mara ya kwanza kinakuwa cha kipekee na huenda taji hilo ni gumu zaidi kuweza kulishinda.
Mafanikio ya Bayer pia yanakuwa yamefuta utawala wa Bayern ambayo msimu huu ilikuwa ikiwania kuweka rekodi ya kulibeba taji la Bundesliga kwa mara ya 12 mfululizo ikiwa kwa sasa ina rekodi ya kulibeba taji hilo mara 11 mfululizo.
Bayern wanaoshika nafasi ya pili katika ligi hiyo pamoja na Stuttgart iliyo nafasi ya tatu wote wameachwa na Bayer kwa tofauti ya pointi 16.
Mafanikio ya Alonso katika Bayer yalianza kuonekana tangu Oktoba 2022 alipojiunga na timu hiyo katika msimu wa 2022-23 akiikuta katika nafasi ya pili kutoka mkiani lakini akapambana hadi kuipandisha kwenye nafasi ya sita.
Katika msimu huu wa 2023-24, Alonso aliendelea kudhihirisha ubora wake baada ya kuwasajili Boniface, Xhaka, Alejandro Grimaldo na Jonas Hofmann ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yanayoonekana sasa.