Rio de Janeiro, Brazil
Mwanasoka nyota wa zamani wa klabu za Real Madrid na Man City, Robinho hatimaye ameanza kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka tisa jela nchini Brazil kwa kosa la kumbaka msichana mmoja nchini Italia.
Katika hali ya kusikitisha, Robinho, 40, jana Alhamisi alionekana akitoka kwenye makazi yake maeneo ya Santos, nje kidogo ya mji wa Sao Paulo na kupakiwa kwenye gari jeusi la polisi.
Uamuzi wa kumfanya nyota huyo wa zamani wa klabu ya Santos na timu ya taifa ya Brazil kuanza kutumikia adhabu hiyo sasa ni baada ya kushindwa katika mpango wake wa kuendelea kuwa huru wakati rufaa yake ikisikilizwa.
Adhabu hiyo imekuja baada ya Mahakama Kuu Brazil kuamua juzi Jumatano kuwa mchezaji huyo ni lazima atumikie adhabu ya kosa la kubaka baada ya kukutwa na hatia mwaka 2017 na mahakama ya nchini Italia.
Awali Robinho alipewa kifungo cha miaka tisa jela nchini Italia kwa kushiriki na vijana wenzake katika tukio la kumbaka msichana huyo mwaka 2013 wakati huo akiichezea AC Milan.
Mawakili wa Robinho walikata rufaa na kutaka mteja wao awe huru wakati wote wa rufaa hiyo na kutaka shauri hilo lisikilizwe upya nchini Brazil kwa sababu hiyo ni nchi yenye mamlaka yake.
Jaji mmoja katika kujenga hoja za kuhakikisha Robinho anahukumiwa nchini Brazil alisema kwamba Brazil haiwezi kuwa sehemu ya watenda makosa ya jinai kuhifadhiwa.
Katika utetezi wake, Robinho alikana kufanya kosa lolote na kwamba kulikuwa na makubaliano na msichana aliyedai kubakwa.
Kimataifa Robinho aanza kutumikia kifungo miaka tisa jela
Robinho aanza kutumikia kifungo miaka tisa jela
Read also
